Alan Shearer ampa maelekezo Tuchel kuelekea mchezo dhidi ya Panama
Mabadiliko ya lazima kwa Tuchel
Gwiji wa soka la England, Alan Shearer, ametoa ushauri mzito kwa kocha Thomas Tuchel kuelekea mchezo wao wa Kombe la Dunia dhidi ya Panama. Shearer anaamini kuwa kikosi cha ‘Three Lions’ kinahitaji kufanyiwa marekebisho ya haraka baada ya kuonyesha kiwango kisichoridhisha katika mchezo wao wa hivi karibuni dhidi ya Ghana uliomalizika kwa sare tasa.
Baada ya kuanza vyema kwa ushindi wa 4-2 dhidi ya Croatia, England walionekana kupata wakati mgumu kuvunja ngome ya Ghana, jambo lililomfanya Shearer kutilia shaka ubunifu wa timu hiyo.
Hakuna haja ya hofu, lakini mabadiliko yanahitajika
Licha ya kukosoa kiwango cha timu hiyo, Shearer amesisitiza kuwa hakuna haja ya mashabiki kuwa na hofu kubwa. Anaamini kuwa lengo la kuongoza kundi bado lipo mikononi mwao, lakini mabadiliko ya kimbinu ni lazima yafanyike ili kuleta kasi zaidi.
“Nilitegemea kuona England ikicheza kwa imani kubwa, kasi na utulivu dhidi ya Ghana, lakini ilikuwa kinyume chake. Hakuna utofauti, kila kitu kilikuwa cha kawaida, pasi zilikuwa za pembeni au nyuma tu,” alisema Shearer.
Mapendekezo ya Shearer kwa Tuchel
Shearer anaamini Tuchel anapaswa kufanya angalau mabadiliko manne katika kikosi chake ili kuongeza tempo ya mchezo. Mchambuzi huyo anapendekeza mabadiliko yafuatayo:
- Ulinzi: Kumrudisha John Stones kuchukua nafasi ya Konsa ili kuimarisha ushirikiano na Guehi, pamoja na kumrudisha Nico O’Reilly kwenye nafasi ya beki wa kushoto.
- Mashambulizi: Kubadilisha mawinga kwa kuwaondoa Anthony Gordon na Noni Madueke, na kuingiza Bukayo Saka na Marcus Rashford.
Kujiamini dhidi ya Panama
Kuhusu mchezo ujao dhidi ya Panama, Shearer anaamini kuwa timu hiyo itatoka na matokeo mazuri iwapo watafuata maelekezo ya kiufundi na kucheza kwa ujasiri zaidi wanapokuwa na mpira.
“Lazima wawe na ujasiri. Wakiwa na nafasi ya kuingiza mipira kwenye kisanduku, lazima wafanye hivyo kwa usahihi. Natabiri mabadiliko haya yataleta nguvu mpya na tutashinda 2-0 au 3-0 dhidi ya Panama,” alimalizia Shearer.
England wanasubiri kuona kama Tuchel atapokea ushauri huu ili kuhakikisha wanapata pointi tatu muhimu zinazoweza kuwapa tiketi ya kutinga hatua inayofuata kwa kishindo.