Alejandro Balde kuanza kulegeza kamba, huenda akajiunga na Manchester United
Balde huenda akatimkia Old Trafford
Beki wa kushoto wa Barcelona, Alejandro Balde, sasa anaonekana kubadili msimamo wake kuhusu hatima yake ndani ya klabu hiyo ya Camp Nou. Inaripotiwa kuwa mchezaji huyo ameanza kuona uwezekano wa kuondoka kufuatia ofa rasmi iliyowasilishwa na Manchester United.
Baada ya kukamilisha usajili wa Carlos Baleba akitokea Brighton, Manchester United inaonekana bado haijatosheka na inahitaji kuongeza beki mwingine wa kushoto ili kukamilisha kikosi chao cha msimu huu. Ingawa walikuwa wakimnyatia Lewis Hall wa Newcastle, mipango hiyo imekwama kutokana na Newcastle kugoma kumuuza mchezaji huyo.
Uamuzi wa Hansi Flick wazua minong’ono
Hali imekuwa ya sintofahamu zaidi baada ya Balde kuachwa nje ya kikosi kilichosafiri kwenda kucheza na Elche, mchezo ambao Barcelona walishinda mabao 5-0. Ingawa kocha Hansi Flick amedai kuwa alimuacha mchezaji huyo kwa sababu hakuwa katika kiwango cha asilimia 100, watu wa karibu na beki huyo wanaona hilo kama ishara ya wazi kuwa klabu haimuhitaji tena.
Akizungumzia hali hiyo, Fabrizio Romano amebainisha kuwa:
Barcelona wapo tayari kumuuza Balde iwapo watapata ofa nzuri. Hata hivyo, Balde mwenyewe hajamua kuondoka kwa shinikizo, isipokuwa anahitaji ofa ya timu kubwa na inayolingana na hadhi yake.
Ofa ya Manchester United mezani
Taarifa kutoka Cadena Ser zinasema kuwa Balde ameanza kuwa na shaka na maisha yake ya baadaye Barcelona. Ingawa hajajulishwa rasmi kama hayupo kwenye mipango ya kocha, ofa nzito kutoka Manchester United imempa wakati mgumu wa kufikiria maamuzi yake ya baadaye.
Changamoto kubwa iliyopo kwa sasa ni mshahara mkubwa anaolipwa Balde huko Barcelona, jambo ambalo Manchester United inabidi ilipatie ufumbuzi katika mazungumzo yao na wakala wa mchezaji huyo, Jorge Mendes.
Hansi Flick amekuwa akisisitiza mara kwa mara kuwa anatarajia kiwango cha juu cha ushindani na nidhamu kutoka kwa Balde. Sasa macho yote yanabaki kwa mchezaji huyo na klabu yake kuona kama safari yake ya kwenda England itatimia kabla ya dirisha la usajili kufungwa.