Alexis Mac Allister aipiga chini Manchester City, athibitisha kusalia Liverpool
Mac Allister hataki kutoka Anfield
Kiungo nyota wa Liverpool, Alexis Mac Allister, ametoa msimamo wake wa kusalia katika klabu hiyo baada ya kuhusishwa na mpango wa kutaka kujiunga na mabingwa wa Premier League, Manchester City.
Manchester City walikuwa wakimfanya mchezaji huyo wa kimataifa wa Argentina kuwa mbadala wa Enzo Fernandez, ambaye klabu yake ya Chelsea imeweka dau la paundi milioni 120 ili kumwachia. Hata hivyo, jaribio la City kumnasa Mac Allister limekwama mapema baada ya mchezaji huyo kuonyesha kutokuwa na nia ya kuondoka.
Ujumbe wa baba mzazi
Baba wa mchezaji huyo, Carlos Mac Allister, ambaye pia ni mchezaji wa zamani, amethibitisha kuwa mwanawe hana mpango wowote wa kutafuta changamoto mpya nje ya Anfield kwa sasa. Katika kauli iliyowekwa wazi na mwandishi Fabrizio Romano, alisema:
“Mwanangu atasalia Liverpool. Hatujajadiliana kuhusu uwezekano wowote wa yeye kuondoka klabuni hapo msimu huu wa joto.”
Kuvutiwa na Andoni Iraola
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa sababu kuu ya Mac Allister kuamua kubaki ni imani yake kwa kocha mpya wa Liverpool, Andoni Iraola. Licha ya msimu wa 2025/26 kuwa mgumu kwa kiungo huyo, anaamini kuwa falsafa ya Iraola itamfaa na kumpa nafasi kubwa ya kuonyesha uwezo wake uwanjani.
Inaelezwa kuwa Mac Allister anafurahia sana mazingira ya sasa klabuni hapo na anatazamia kuanza msimu mpya akiwa na matumaini makubwa chini ya utawala wa kocha huyo mpya.
Liverpool wapanga kumuongezea mkataba
Kutokana na umuhimu wake, Liverpool nao hawako tayari kumuacha kiungo huyo aondoke. Klabu hiyo imepanga kuanza mazungumzo ya kumuongezea mkataba mpya baadaye mwaka huu ili kumfanya aendelee kuwa nguzo muhimu katika kikosi chao.
Mkataba wa sasa wa Mac Allister unasalia na kipindi cha miaka miwili, lakini uongozi wa Liverpool unataka kumpa ofa iliyo bora zaidi ili kutambua mchango wake mkubwa kikosini. Kwa sasa, mchezaji huyo ameelekeza nguvu zake zote katika mazoezi na kujiandaa na msimu mpya chini ya Iraola.