Andy Gray ahoji kiwango cha Milos Kerkez Liverpool
Shinikizo kwa Milos Kerkez Anfield
Beki wa kushoto wa Liverpool, Milos Kerkez, amejikuta kwenye wakati mgumu baada ya kuonyesha kiwango kisichoridhisha katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Ulaya dhidi ya Atletico Madrid uliomalizika kwa Liverpool kushinda 2-1.
Mchambuzi wa soka, Andy Gray, ambaye alikuwa akifuatilia mchezo huo kwa karibu, amedai kuwa mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 22 anaonekana kushindwa kumudu presha ya kuchezea klabu kubwa kama Liverpool tangu asajiliwe kwa ada ya pauni milioni 40 kutoka Bournemouth mwaka 2025.
Kosa la goli la Atletico
Katika mchezo huo, Atletico Madrid walitangulia kupata bao kupitia kwa Marcos Llorente dakika ya 17. Kerkez alionekana kuhusika moja kwa moja na goli hilo baada ya kushindwa kuizuia pasi iliyomfikia Llorente, jambo ambalo lilimfanya Gray kutoa dukuduku lake.
“Kerkez niliyemuona Bournemouth siyo yule ninayemuona hapa sasa hivi. Sikuwa nashangaa Liverpool walipomsajili kwa sababu alikuwa mmoja wa mabeki bora zaidi ligini kwa mbali. Lakini bado hajajipata kwenye nafasi yake ile ile aliyokuwa nayo awali,” alisema Gray.
Gray aliongeza kuwa wakati mwingine changamoto inaweza kuwa ukubwa wa klabu husika kwa mchezaji fulani.
“Sijui kama… wakati mwingine klabu inakuwa kubwa mno kwa watu. Natumai si hivyo kwa Kerkez, kwa sababu nampenda sana kama mchezaji na nimefurahi kidogo kuona alihusika kwenye bao la kusawazisha,” aliongeza mchambuzi huyo.
Maoni ya Jamie Carragher
Sio Andy Gray pekee anayeonekana kuwa na shaka na beki huyo. Hivi karibuni, gwiji wa Liverpool, Jamie Carragher, naye alitoa maoni makali akimfananisha Kerkez na Darwin Nunez kwa namna anavyocheza kwa kasi isiyo na utulivu.
Carragher alieleza kuwa Kerkez ana tatizo la kufanya kila kitu kwa mbio za ‘kilomita 100 kwa saa’ bila kuwa na utulivu wa kufikiri au kubadili mwelekeo wa mchezo. Licha ya changamoto hizo, inaonekana Liverpool bado inamuamini kijana huyo kama chaguo la kwanza katika nafasi ya beki wa kushoto baada ya Andy Robertson kuondoka klabuni hapo.
Kwa sasa, mashabiki wa ‘The Reds’ wanaendelea kumsubiri Kerkez kuonyesha kiwango kile kilichomfanya asajiliwe kwa fedha nyingi, huku shinikizo likiongezeka kila siku kutokana na matarajio makubwa yaliyopo klabuni hapo.