Wachezaji wa Argentina washangazwa na maamuzi ya Thomas Tuchel dhidi ya England
Mbinu za Tuchel zawaacha Argentina vinywa wazi
Maumivu ya kuondolewa katika hatua ya nusu fainali ya Kombe la Dunia bado yanawatafuna mashabiki wa England, kufuatia kipigo cha mabao 2-1 dhidi ya Argentina katika mchezo uliopigwa Jumatano iliyopita. Hata hivyo, taarifa mpya zimebainisha kuwa hata wapinzani wao, Argentina, walishangazwa na jinsi kocha wa England, Thomas Tuchel, alivyocheza mchezo huo.
Inadaiwa kuwa wachezaji wa Argentina walikuwa katika hali ya tahadhari kubwa, wakitarajia kuingizwa kwa mastaa wa Arsenal, Bukayo Saka na Noni Madueke, hasa kipindi cha mapumziko. Kocha Lionel Scaloni na benchi lake la ufundi walikuwa wamejiandaa kupambana na kasi ya wachezaji hao, wakijua kuwa walikuwa hatari zaidi pindi mchezo unapoanza kuwa wazi.
Scaloni alitarajia mashambulizi zaidi
Badala ya kuingiza wachezaji wenye kasi, Tuchel alichagua kufanya mabadiliko ya kiulinzi baada ya bao la Anthony Gordon katika dakika ya 55. Hatua hii ilionekana kama jaribio la kutaka kulinda goli hilo, lakini matokeo yake yakawa tofauti.
Akielezea hali hiyo, ripoti moja ilibainisha:
Scaloni na wasaidizi wake walikuwa wakijipanga kwa ajili ya Saka au Madueke kuingia uwanjani, lakini walishangazwa kuona Tuchel akileta wachezaji wenye mtazamo wa kujilinda. Hii ilimfanya Scaloni ajihisi huru kushambulia zaidi, ikiwemo kumuingiza Lautaro Martinez ambaye ndiye aliyekuwa mfungaji wa bao la ushindi.
Wachezaji wa England nao wanalalamika
Sio Argentina pekee waliohoji mbinu za kocha huyo, kwani hata ndani ya kambi ya England hali sio shwari. Taarifa kutoka BBC Sport zinaeleza kuwa wachezaji wasiopungua watatu waandamizi wa timu hiyo wameonyesha kutoridhishwa na maelekezo ya Tuchel katika dakika za mwisho za mchezo.
Wachezaji hao wanaamini kuwa uamuzi wa kocha kuirudisha timu nyuma baada ya kuongoza ndio uliowa gharimu, kwani uliiruhusu Argentina kuongeza presha na hatimaye kupata mabao kupitia kwa Enzo Fernandez na Lautaro Martinez.
Ingawa wachezaji wanakiri kuwa wakati mwingine ni silika ya kawaida kujilinda unapokuwa mbele kwa goli, wanahisi kuwa mabadiliko ya kimbinu ya Tuchel yaliwavua nguvu zao za mashambulizi ya kushtukiza na kuwapa wapinzani nafasi ya kumiliki mchezo kikamilifu.