Skip to content

Argentina wampumua Lionel Messi, nyota watatu tayari kwa nusu fainali dhidi ya England

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 13 Julai 2026 · 2 min read
argentina lionelmessi england kombeladunia nusufainali
Argentina wampumua Lionel Messi, nyota watatu tayari kwa nusu fainali dhidi ya England

Habari njema kwa Argentina kuelekea ‘vita’ ya nusu fainali

Kikosi cha Argentina kimepokea habari njema sana kuelekea mchezo wao wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya England utakaopigwa huko Atlanta siku ya Jumatano. Nyota watatu muhimu, Lionel Messi, beki Cristian Romero, na kiungo Leandro Paredes, wamethibitishwa kuwa fiti na wapo tayari kuivaa ‘Three Lions’.

Argentina, ambao ni mabingwa watetezi, walilazimika kucheza dakika 120 za nyongeza katika hatua ya robo fainali dhidi ya Uswisi. Katika mchezo huo, walihitaji juhudi za washambuliaji Julian Alvarez na Lautaro Martinez ili kuvuka na kufika nusu fainali, baada ya mchezo kuwa mgumu kuliko ilivyotarajiwa.

Hofu iliyotanda kikosini

Kuelekea mchezo wa nusu fainali, kulikuwa na hofu kubwa kufuatia uchovu uliokuwa dhahiri kwa wachezaji. Kulingana na taarifa za kituo cha TyC Sports cha Argentina, mchanganyiko wa joto kali, safari ndefu, na mfumo wa Kombe la Dunia la mwaka huu wenye timu 48, umekuwa na athari kubwa kwa kikosi cha kocha Lionel Scaloni.

Katika mchezo dhidi ya Uswisi, Romero na Paredes walionekana kupata maumivu na kulazimika kubadilishwa wakati wa muda wa nyongeza. Hali kadhalika, Lionel Messi alipata pigo baada ya kugongana na Granit Xhaka, tukio lililomfanya apate jeraha jichoni na kuhitaji huduma ya kwanza uwanjani.

Wachezaji wote wako salama

Licha ya sintofahamu hiyo, taarifa kutoka kambi ya Argentina zinasema kuwa hakuna mchezaji yeyote aliyepata jeraha la kudumu. Romero na Paredes walitoka uwanjani wakiwa wamechoka sana, lakini vipimo vinaonyesha kuwa hawana matatizo yoyote ya kimwili. Kuhusu Messi, maumivu aliyokuwa nayo yaliisha muda mfupi baada ya mchezo kumalizika.

Kwa sasa, Argentina inaendelea na mazoezi yao kujiandaa kwa safari ya kwenda Atlanta. Ushindi katika mchezo huu utawapeleka moja kwa moja kwenye fainali ya Jumapili, ambapo watakutana na mshindi kati ya Ufaransa na Uhispania.

Hali ilivyo upande wa England

Kwa upande wa England, kocha Thomas Tuchel naye anaonekana kuwa na ahueni. Kiungo Declan Rice, ambaye alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa kabla ya mchezo dhidi ya Norway, anatarajiwa kuwa fiti, huku Ezri Konza naye akiwa amepona maumivu ya misuli aliyopata hivi karibuni. Hii inatoa picha kuwa pande zote mbili zitaingia uwanjani zikiwa na vikosi vyao kamili kwa ajili ya mchezo huu mkubwa.