Arsenal yafanya kweli: Bruno Guimaraes karibu kutua Emirates, mipango ya kusajili beki mpya mbioni
Guimaraes mbioni kujiunga na Arsenal
Klabu ya Arsenal inaonekana kuwa na mikakati mizito katika dirisha hili la usajili, huku ikipanga kuleta sura mpya mbili kubwa katika kikosi cha Mikel Arteta. Kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, ndiye chaguo namba moja la kocha huyo na inaelezwa kuwa dili hilo limefikia hatua za mwisho kabisa.
Mtaalamu wa masuala ya usajili barani Ulaya, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa mazungumzo kati ya pande hizo mbili yamepamba moto na ni suala la muda tu kabla ya kukamilisha kila kitu.
“Kuhusu kiungo? Kuna mtu mmoja tu waliyemlenga: Bruno Guimarães. Ni kama dili lililokamilika kwa Gunners, mazungumzo kati ya Newcastle na Arsenal yamefikia hatua kubwa. Wapo kwenye hatua za mwisho za maelewano kabla ya kupanga vipimo vya afya na kusaini nyaraka za mkataba,” alisema Romano.
Arteta anaelezwa kuwa na shauku kubwa ya kumpata nyota huyo wa Brazil ambaye amekuwa kwenye rada zake kwa muda mrefu ili kuimarisha safu yake ya kiungo.
Vinicius Junior na ndoto za Emirates
Ukiacha Guimaraes, Arsenal inahusishwa na mpango mkubwa zaidi wa kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior. Ingawa mchezaji huyo bado anafanya mazungumzo ya mkataba mpya na klabu yake ya sasa, taarifa kutoka Hispania zinaashiria kuwa uongozi wa Real Madrid uko tayari kumuachia ikiwa makubaliano hayatafikiwa, ili wasimpoteze bure msimu ujao.
Beki mpya ajiongeza kwenye orodha ya Arteta
Katika hali ya kushtukiza, Arsenal pia inatazamia kuimarisha safu ya ulinzi. Hii inatokana na hali ya beki wake tegemeo, William Saliba, ambaye anasumbuliwa na majeraha ya mgongo aliyoyapata wakati akiwa na timu ya taifa ya Ufaransa kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
Ingawa haikuhitaji kufanyiwa upasuaji, Saliba atakuwa nje ya uwanja kwa miezi kadhaa, hali inayomlazimisha Arteta kutafuta mbadala wa haraka. Jina la beki wa Aston Villa, Ezri Konsa, limekuwa likitajwa mara kwa mara kama mlengwa mkuu wa Arsenal ili kuziba pengo hilo.
“Arsenal inatarajiwa kuwa moja ya klabu zenye shughuli nyingi zaidi katika Ligi Kuu ya England. Mpango wao ni kuongeza mshambuliaji mwingine, na wanaweza hata kusajili beki mpya wa kati kutokana na matatizo ya mgongo yanayomkabili Saliba,” aliongeza Romano.
Ni dhahiri kuwa Arsenal haijaridhika na kikosi chake cha sasa na inakusudia kufanya maboresho makubwa ili kuendelea kupambana kwenye ligi na michuano mingine msimu ujao.