Arsenal kumpiga bei Noni Madueke, Raphinha na Ngumoke watajwa
Madueke kuondoka Emirates?
Kuelekea dirisha dogo la usajili la mwezi Januari, kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, anaripotiwa kuwa tayari kuachana na winga wake, Noni Madueke. Mchezaji huyo wa kimataifa wa Uingereza, ambaye alijiunga na Arsenal mwaka 2025 kwa ada ya pauni milioni 52 akitokea Chelsea, amepoteza nafasi yake katika kikosi cha kwanza.
Tangu kurejea kwa Bukayo Saka, Madueke amekuwa akisota benchi huku akicheza mechi mbili pekee kama mchezaji wa akiba katika michezo minne ya kwanza ya Ligi Kuu ya England (Premier League) msimu huu. Hali hii imeibua tetesi kuwa huenda akaondoka ili kutafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara.
Juventus na Atletico Madrid wanachungulia
Taarifa za ndani zinaeleza kuwa klabu za Juventus kutoka Italia na Atletico Madrid ya Hispania zimeanza kufuatilia kwa karibu mwenendo wa Madueke. Inadaiwa kuwa klabu hizo zinapendelea kumsajili kwa mkopo kwanza, huku kukiwa na uwezekano wa kuweka kipengele cha kumnunua moja kwa moja baadaye.
Ingawa bado hakuna mazungumzo rasmi yaliyofanyika, inafahamika kuwa Atletico Madrid wanavutiwa na kasi na uwezo wa mchezaji huyo kushambulia moja kwa moja, sifa ambazo Diego Simeone anaamini zinaweza kuongeza makali kwenye kikosi chake.
Raphinha na Ngumoha kwenye rada
Katika hatua nyingine, Arsenal inatajwa kuwa moja ya klabu nne zinazotaka kumvuta Raphinha kutoka Barcelona. Inasemekana kuwa Arsenal wapo tayari kumpa mshahara mkubwa staa huyo wa Brazil ambaye kwa sasa ni nahodha wa klabu hiyo ya Catalan.
Hata hivyo, Raphinha anaonekana kutokuwa na haraka ya kuondoka, huku akisisitiza kuwa anafurahia maisha yake Hispania. Lengo lake kubwa kwa sasa ni kuona mkataba wake unaboreshwa ili awe miongoni mwa wachezaji wanaolipwa mishahara mikubwa zaidi klabuni hapo, sawa na Lamine Yamal.
Kuhusu winga wa Liverpool, Rio Ngumoha, mtaalamu wa masuala ya usajili Fabrizio Romano ameweka wazi kuwa kwa sasa Liverpool hawana mpango wa kumuuza kijana huyo.
“Liverpool wamekuwa na msimamo uleule, mchezaji huyo hauzwi. Wanamwamini Rio kama sehemu ya mustakabali wa klabu,” alisema Romano.
Kwa sasa, mashabiki wa Arsenal wanasubiri kuona hatua gani Arteta atachukua Januari, kwani kila mchezaji anayeondoka atahitaji kuzibwa nafasi yake kwa ubora zaidi.