Arsenal wagoma kumuuza Myles Lewis-Skelly kwa Manchester United
Arsenal wamkataa beki wao kwa United
Klabu ya Arsenal imeweka msimamo mkali kuhusu mustakabali wa chipukizi wao Myles Lewis-Skelly, huku wakisisitiza kuwa hawana mpango wowote wa kumuuza mchezaji huyo kwa mahasimu wao Manchester United.
Ripoti za hivi karibuni zilionyesha kuwa Manchester United walikuwa wanavutiwa na huduma za beki huyo ambaye pia ana uwezo wa kucheza nafasi ya kiungo cha kati. Hata hivyo, Arsenal imekataa katakata wazo hilo, ikionyesha bayana kuwa haitaki kuwapa wachezaji wake wapinzani wao wa moja kwa moja kwenye ligi.
Kocha Mikel Arteta anaonekana kumthamini sana Lewis-Skelly kama sehemu muhimu ya mradi wake kwa msimu wa 2026-27. Imani hii inatokana na kiwango bora alichokionyesha msimu uliopita, hasa alipochezeshwa katikati ya uwanja.
Bruno Guimaraes atua Emirates
Uamuzi huu wa kumbakiza Lewis-Skelly unakuja wakati Arsenal ikimalizia kukamilisha usajili mkubwa wa kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes. Mchezaji huyo anatarajiwa kujiunga na washika mitutu hao kwa ada ya paundi milioni 75.
Habari za kukamilika kwa dili hilo zimeleta shangwe kwa mashabiki wa Arsenal, kwani Guimaraes anaonekana kama kipande muhimu kilichokuwa kimepungua kwenye kikosi cha Arteta. Taarifa kutoka kwa mwandishi wa Sky Sports, Keith Downie, zinaeleza kuwa Newcastle hawakutaka kumuuza nyota huyo, lakini walilazimika kufuata matakwa ya mchezaji mwenyewe ambaye alitaka kuondoka ili kupata nafasi ya kushinda mataji makubwa.
“Newcastle hawakutaka kumuuza na walikuwa na hamu kubwa ya kumbakiza Bruno Guimaraes. Kama angeamua kubaki, Newcastle wangakataa ofa yoyote kutoka kwa Arsenal au klabu nyingine yoyote,” ilieleza ripoti hiyo.
Ujenzi wa kikosi unaendelea
Arsenal imekuwa na dirisha la usajili lenye pilikapilika nyingi msimu huu. Mbali na Guimaraes, tayari wamefanikiwa kuwasajili Illan Meslier na Christos Tzolis, huku pia wakikamilisha uhamisho wa kudumu wa Piero Hincapie aliyekuwa kwa mkopo.
Kwa upande wa Manchester United, nia yao ya kumsajili Lewis-Skelly ilikuwa ni kuimarisha eneo la beki wa kushoto. Hata hivyo, kwa msimamo huu wa Arsenal, inaonekana United watalazimika kuelekeza nguvu zao kwingine kwani vijana wa Arteta hawauzwi kwa wapinzani wa karibu.