Arsenal wajiondoa kwenye mbio za kumsajili Bradley Barcola
Arsenal watoa uamuzi mzito kuhusu Barcola
Klabu ya Arsenal imethibitisha kuwa haitafanya jaribio lolote la kumsajili winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola, katika siku hizi za mwisho za dirisha la usajili. Hatua hii inaifanya Liverpool kubaki katika nafasi nzuri ya kumsajili mchezaji huyo.
Awali, Mikel Arteta alikuwa amemweka Barcola kwenye orodha yake ya wachezaji anaowataka ili kuongeza nguvu katika eneo la ushambuliaji, hasa baada ya mabadiliko kadhaa yaliyofanyika kikosini, ikiwemo ujio wa Christos Tzolis na uwezekano wa Gabriel Martinelli kuondoka kuelekea Al-Hilal.
Kwa nini Arsenal wamejitoa?
Sababu kubwa ya Arsenal kujiondoa katika mbio hizo ni gharama kubwa inayotakiwa na PSG. Ingawa PSG wameshusha bei ya mchezaji huyo kutoka Euro milioni 170 hadi milioni 140, Arsenal bado wanaona gharama hiyo ni kubwa mno kwa mchezaji ambaye hana uhakika wa kuanza kila mechi kikosini mwa miamba hiyo ya Ufaransa.
Arsenal wamekuwa wakitafuta mbadala wa wachezaji kama Morgan Rogers na Vinicius Junior, lakini sasa wanaonekana kubadili mwelekeo huku kukiwa na uvumi wa huenda wakamrudia Nico Williams kama chaguo jingine.
Liverpool katika nafasi nzuri
Wakati Arsenal wakijiondoa, Liverpool wameendelea kuwa imara katika mazungumzo na PSG. Ripoti zinaeleza kuwa mazungumzo kati ya wakurugenzi wa pande zote mbili yanaendelea vizuri nyuma ya pazia.
“Liverpool na PSG wanaendelea na mawasiliano ya moja kwa moja kila siku. Huu ni usajili ambao Liverpool wanataka kuukamilisha katika siku chache zijazo, na matarajio yangu ni kuona Liverpool wakijituma kikamilifu kumnasa Barcola,” alisema mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano.
Liverpool wamekuwa tayari kuweka dau kubwa ili kupata huduma ya winga huyo, na inaonekana wako tayari kufika kiasi cha pauni milioni 120 kilichotajwa. Ikiwa dili hili litakamilika, Liverpool bado wataendelea kutafuta mshambuliaji mwingine ikiwa Cody Gakpo ataondoka klabuni hapo kuelekea Tottenham au Manchester City.