Skip to content

Arsenal walivyopigwa bao na Chelsea kwenye usajili wa Morgan Rogers

SokaNews
Updated: Published: Jumatatu, 20 Julai 2026 · 2 min read
arsenal chelsea morganrogers usajili fabrizioromano yandiomande
Arsenal walivyopigwa bao na Chelsea kwenye usajili wa Morgan Rogers

Mshangao kwa Arsenal

Klabu ya Arsenal imepata pigo kubwa katika dirisha hili la usajili baada ya Chelsea kuingilia kati na kufanikisha dili la kumsajili winga machachari wa Aston Villa, Morgan Rogers. Tukio hili limeelezwa na mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, kama “mshangao mkubwa” kwa washika bunduki hao wa London.

Inaelezwa kuwa Arsenal walikuwa wakiongoza mbio za kumnasa mchezaji huyo wa kimataifa wa England kwa muda mrefu, na hata walishafikia makubaliano ya awali kuhusu maslahi binafsi ya mchezaji huyo. Kocha Mikel Arteta alikuwa akimhitaji Rogers kama mbadala mahiri anayeweza kucheza nafasi yoyote katika safu ya ushambuliaji au nyuma ya mshambuliaji.

Chelsea wajiongeza kimaslahi

Chelsea walifanya maamuzi ya haraka kwa kukubali kulipa kitita cha pauni milioni 117, fedha ambazo Arsenal walikuwa hawako tayari kuzifikia. Wakati Arsenal wakipanga kutoa ofa ya juu kabisa ya pauni milioni 100, Chelsea waliamua kuweka dau mezani ili kumaliza kazi hiyo ndani ya saa 24.

Akizungumzia dili hilo, Romano alisema:

“Kwa Arsenal, huu ni mshangao mkubwa kwa sababu sasa wanalazimika kurejea sokoni kutafuta mbadala. Mikel Arteta alikuwa na mazungumzo ya moja kwa moja na Morgan Rogers kwa miezi kadhaa na alikuwa mlengwa mkuu.”

Rogers amesaini mkataba wa miaka sita, huku kukiwa na chaguo la kuongeza msimu mwingine, hatua inayoonekana kama uwekezaji mkubwa kwa Chelsea.

Arsenal wahamishia nguvu kwa Yan Diomande

Baada ya kupoteza nafasi ya kumnasa Rogers, Arsenal sasa wameelekeza macho yao kwa winga wa RB Leipzig, Yan Diomande. Hata hivyo, dili hili nalo linaonekana kuwa na ushindani mkali.

Paris Saint-Germain (PSG) bado wanaonekana kuwa mstari wa mbele kwa kuwa tayari wameshafikia makubaliano na mchezaji mwenyewe tangu wiki kadhaa zilizopita. Changamoto iliyopo kwa PSG ni kufikia muafaka wa kifedha na klabu ya RB Leipzig.

Romano aliongeza kusema:

“Arsenal wamefanya uchunguzi wa hivi karibuni, na kuna klabu nyingine pia zinafuatilia hali hiyo nyuma ya pazia. Kwa sasa, PSG wanatakiwa kuharakisha kukamilisha dili hilo na Leipzig ili wasije wakapoteza fursa kama ilivyotokea kwa Arsenal na Rogers.”

Ni wazi kuwa Arsenal wapo katika wakati mgumu wa kutafuta mchezaji atakayeziba pengo hilo, huku soko la usajili likizidi kuwa na ushindani mkali.