Arsenal yajipanga kutuma ofa ya pauni milioni 70 kwa Bruno Guimaraes
Mvutano wa usajili wa Bruno Guimaraes
Klabu ya Arsenal inaendelea kuonyesha nia thabiti ya kumsajili kiungo wa Newcastle United, Bruno Guimaraes, huku kukiwa na ripoti kwamba wanaandaa ofa mpya ya pauni milioni 70. Hii itakuwa ni hatua ya tatu ya Gunners baada ya majaribio yao ya awali ya pauni milioni 55 na 65 kukataliwa na klabu hiyo ya St James’ Park.
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa Arsenal tayari wamekubaliana na mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 28 kuhusu maslahi binafsi. Inasemekana kuwa Guimaraes ameshaweka wazi nia yake ya kutaka kuondoka Newcastle ili kujiunga na mradi wa Mikel Arteta, japo anataka kufanya hivyo kwa njia ya heshima bila kuharibu uhusiano wake na klabu yake ya sasa.
Newcastle bado wagumu
Licha ya presha kubwa kutoka kwa Arsenal na hamu ya mchezaji mwenyewe, Newcastle United wamesimama kidete wakisisitiza kuwa hawana mpango wa kumuuza nyota huyo. Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa ofa ya pauni milioni 70 bado haitoshi kuwashawishi wamiliki wa Newcastle kubadili msimamo wao.
Mwandishi wa habari Lee Ryder, ambaye anafuatilia kwa karibu taarifa za Newcastle, amesisitiza kuwa kiasi hicho cha pesa ni “jambo lisilowezekana” kwa klabu hiyo kuachana na kiungo huyo. Newcastle wanatarajia mchezaji huyo kuripoti kikosini kwa ajili ya kambi ya mazoezi huko La Manga, jambo linaloashiria kuwa hawajakata tamaa ya kumbakiza.
“Arsenal wako tayari kutuma ofa mpya. Wanataka kwenda kwa Bruno na wana makubaliano kamili naye. Mkataba umekamilika, Bruno amesema ndiyo kwa mradi wa Arsenal, lakini anataka kuwa na heshima kwa Newcastle,” alisema Romano.
Nini kinafuata?
Arsenal wako katika nafasi ngumu. Kwa upande mmoja, Mikel Arteta anaripotiwa “kushinikiza kwa nguvu” ili kukamilisha dili hilo, lakini klabu imesema haitafanya maamuzi ya kukurupuka au kutoa pesa nyingi kupita kiasi (overpaying) kwa ajili ya mchezaji mmoja tu.
Itabidi tuone kama Arsenal wataongeza dau hilo ili kufikia kile kinachodhaniwa kuwa bei halisi ya kumng’oa Guimaraes, au kama Newcastle wataendelea kushikilia msimamo wao wa kutomuuza kiungo huyo muhimu katika msimu ujao.