Arsenal yajipanga kunasa saini ya Erling Haaland kama Man City itashushwa daraja
Arsenal yajipanga kwa ajili ya Haaland
Klabu ya Arsenal inaripotiwa kuwa tayari kufanya kile kinachotajwa kama ‘jaribio zito’ la kumsajili mshambuliaji matata wa Manchester City, Erling Haaland, endapo mabingwa hao wa sasa wa England watajikuta wakishushwa daraja kufuatia sakata lao la ukiukaji wa kanuni za matumizi ya fedha (FFP).
Ripoti zimekuwa zikieleza kuwa Manchester City inakabiliwa na tuhuma nzito za ukiukaji wa sheria 114 kati ya 115 walizokuwa wakichunguzwa na Premier League. Ingawa uamuzi rasmi bado haujatolewa, uvumi umekuwa ukienea kuwa klabu hiyo imepatikana na hatia ya mashtaka mengi, jambo linaloweza kupelekea adhabu kali ikiwemo kushushwa daraja.
Ofa ya kihistoria kuwinda nyota
Taarifa kutoka vyanzo mbalimbali zinaeleza kuwa uongozi wa Arsenal chini ya Mikel Arteta tayari umeanza kuweka mikakati ya chini kwa chini, huku wakiwa tayari kufanya uwekezaji mkubwa wa kifedha ili kumnasa mshambuliaji huyo wa Norway ikiwa hali itabadilika katika kambi ya City.
Inaelezwa kuwa Arsenal wamejipanga kufanya kila linalowezekana, wakijaribu kuonyesha nia yao ya kusajili mastaa wakubwa baada ya jaribio lao la hivi karibuni la kutaka kumsajili Vinicius Junior kutoka Real Madrid.
“Ingawa usajili wa Vinicius haukufanikiwa, ilikuwa ni ishara tosha kuwa Arsenal hawaogopi kusajili wachezaji wa daraja la dunia. Ni wazi bado kuna hatua nyingi za kupita kabla ya dili la Haaland kutimia, lakini vyanzo vyetu viko wazi kuwa Arsenal wanapanga kuwepo kwenye mazungumzo na wapo tayari kufanya uwekezaji mkubwa kifedha kama City watapewa adhabu nzito.”
Mustakabali wa Man City shakani
Manchester City kwa sasa wanasubiri matokeo ya mwisho ya uchunguzi huo wa miaka minne. Adhabu zinazoweza kuikabili klabu hiyo ni pamoja na faini kubwa, kufungiwa kusajili, kupokonywa mataji ya Premier League, au hata kufukuzwa kabisa kwenye ligi.
Ikiwa hali hiyo ya kushushwa daraja itatokea, inatarajiwa kuwa nyota wengi wa kikosi cha Pep Guardiola wataondoka, na Haaland anatajwa kuwa mmoja wa wachezaji ambao hawataweza kusalia kwenye klabu hiyo.
Kwa sasa, mashabiki wa soka nchini Uingereza na duniani kote wanasubiri kuona hatma ya kesi hii, huku Arsenal wakionekana kuwa makini kufuatilia kila hatua ili kuona kama wanaweza kunufaika na mgogoro huo kumpata mmoja wa wafungaji bora zaidi duniani kwa sasa.