Arsenal yafanya kasi kumnasa Morgan Rogers, Bradley Barcola nje ya rada
Arsenal yajikita kwa Morgan Rogers
Klabu ya Arsenal imeonekana kuamua kuweka nguvu zake zote katika kumsajili kiungo mshambuliaji wa Aston Villa, Morgan Rogers, katika harakati zao za kujiimarisha kabla ya kuanza kwa msimu mpya wa Ligi Kuu ya England. Mabingwa hao watetezi wameonekana kuharakisha mazungumzo ili kupata saini ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 23.
Mwandishi wa habari za usajili, Fabrizio Romano, amethibitisha kuwa Rogers sasa ndiye mlengwa mkuu wa Arsenal. Hii inakuja wakati klabu hiyo pia ikiwa katika hatua za mwisho za kukamilisha usajili wa winga wa Club Brugge, Christos Tzolis, kwa ada ya takriban pauni milioni 34, ili kuziba pengo la Leandro Trossard aliyejiunga na Fenerbahce.
Changamoto kwa Aston Villa
Kwa upande wa Aston Villa, kocha Unai Emery hatakuwa tayari kumuachia kiungo wake huyo ambaye alikuwa nguzo muhimu msimu uliopita. Rogers alionyesha kiwango bora kwa kufunga mabao 14 na kutoa pasi 12 za mabao, akisaidia timu hiyo kutwaa taji la Europa League na kufuzu kushiriki Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Licha ya Arsenal kufanya mazungumzo ya hali ya juu na wawakilishi wa mchezaji huyo, Aston Villa inaelezwa kuwa na thamani ya takriban pauni milioni 130 kwa nyota huyo ambaye bado ana mkataba wa miaka mitano klabuni hapo. Hii inatarajiwa kuwa sehemu ngumu ya mazungumzo kati ya pande hizo mbili.
Mtazamo wa Rogers kuhusu tetesi za usajili
Kuhusu tetesi za kuondoka, Rogers mwenyewe amewahi kusema kuwa amejifunza kuishi na kelele za sokoni bila kupoteza umakini wake uwanjani. Katika mahojiano kwenye podikasti ya The Rest is Football, alisema:
“Nafikiri mara ya kwanza ilipotokea ilikuwa ni kero na kizuizi. Uko katika nafasi isiyo na raha ambapo hutambui kuwa watu wanakuwekea nia kubwa kiasi hicho. Lakini kadiri unavyozeeka na kupata uzoefu, unajua hilo ni jambo la kawaida na asilimia 95 ya mambo hayo ni kelele tu.”
Aliongeza kuwa, “Unazisikia, bila shaka huwezi kusaidia kutozisikia. Unajua zipo, lakini lazima uzitumie kwa njia chanya. Unajaribu tu kuendelea na mchezo wako na kuzingatia majukumu yako.”
Bradley Barcola si kipaumbele
Wakati kukiwa na taarifa nyingi za usajili, Romano amesisitiza kuwa kwa sasa Arsenal haijafanya mazungumzo yoyote na kambi ya mshambuliaji wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola. Focus ya The Gunners kwa sasa imeelekezwa moja kwa moja kwa Rogers, huku wakijaribu kukamilisha mipango yao ya usajili kabla ya msimu mpya kuanza mwezi ujao.