Arsenal yapaa kileleni katika mbio za kumsajili Bradley Barcola
Vita ya kuwania saini ya Barcola inazidi kushika kasi
Klabu ya Arsenal inatajwa kuwa mstari wa mbele katika mbio za kuwania saini ya winga wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola. Taarifa hii imekuja kama pigo kubwa kwa Liverpool, ambao nao wamekuwa wakimfuatilia kwa karibu nyota huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa ili kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Mohamed Salah.
Baada ya kuondoka kwa Salah mwishoni mwa msimu, Liverpool wamekuwa wakisaka mbadala wake. Ingawa tayari wamemsajili Victor Munoz kutoka Osasuna, inaonekana bado wanahitaji kuongeza nguvu nyingine katika safu yao ya ushambuliaji. Hapo awali, walikuwa wakimtarget Yan Diomande wa RB Leipzig, lakini mchezaji huyo anaonekana kupendelea kujiunga na PSG, hali iliyowalazimisha Liverpool kugeukia vyanzo vingine vya usajili.
Hali ya Barcola pale PSG
Mchambuzi wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, ameweka wazi kuwa kwa sasa Barcola hayupo tena kwenye kundi la wachezaji wasioweza kuuzwa pale PSG. Mazungumzo ya mkataba mpya kati ya pande hizo mbili yamekwama kwa muda mrefu, jambo linalofungua milango kwa klabu nyingine kujaribu bahati zao.
“Barcola ana nafasi kubwa ya kuondoka Paris katika dirisha hili la usajili. Hadi wiki iliyopita alikuwa ‘hagusiki’, lakini sasa mambo yamebadilika. PSG watataka kiasi kikubwa cha pesa, hivyo ni vita ya nani atawasilisha ofa bora,” alisema Romano.
Arsenal wana nafasi kubwa zaidi?
Licha ya Liverpool kuonekana kuhitaji sana winga mpya, mwandishi wa Daily Mail, Lewis Steele, amedokeza kuwa kuna taarifa kutoka ndani ya Arsenal zinazoashiria kuwa ‘The Gunners’ wako mbele zaidi katika kinyang’anyiro hicho.
Ingawa Arsenal wanahusishwa pia na Morgan Rogers, inaonekana Barcola yupo kwenye mipango yao ya muda mrefu. Hata hivyo, bado kuna sintofahamu kama Arsenal wataweza kumudu gharama za usajili wa wachezaji wote wawili ikiwa wataamua kuwasajili kwa pamoja.
Kwa upande wa Liverpool, Steele anaamini kuwa ni lazima wajiongeze:
“Nafikiri ni asilimia 99 kuwa watalazimika kusajili winga mwingine. Huwezi kumuacha mchezaji bora zaidi wa muongo uliopita aondoke bila kuziba pengo lake. Wana fedha za kufanya usajili huo, na wanajua umuhimu wa kufanya hivyo,” aliongeza Steele.
Kwa sasa, mashabiki wa soka wanaendelea kusubiri kuona ni wapi nyota huyu atatua, huku PSG wakitarajiwa kuhitaji ofa nono ili kumwachia winga huyo aliyeng’ara kwenye michuano ya Kombe la Dunia.