Arsenal yamsini Ezri Konsa kwa £55m, Julian Alvarez bado anawaza Barcelona
Arsenal yafunga kazi kwa Ezri Konsa
Klabu ya Arsenal imefanikiwa kukamilisha usajili wa beki kisiki kutoka Aston Villa, Ezri Konsa, kwa dau la pauni milioni 55. Ujio wa mchezaji huyu mwenye umri wa miaka 28 ni ishara tosha kuwa Mikel Arteta anataka kuimarisha safu yake ya ulinzi kwa wachezaji wenye uzoefu wa kutosha kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League).
Kwa mujibu wa taarifa kutoka kwa mwandishi David Ornstein, dili hilo limegawanyika katika ada ya msingi ya pauni milioni 51 na nyongeza ya pauni milioni 4 kulingana na mafanikio ya mchezaji huyo uwanjani. Konsa amesaini mkataba wa miaka minne, huku kukiwa na kipengele cha kuongeza mwaka mwingine mmoja.
Umuhimu wa Konsa kwa Arteta
Uwezo wa Konsa kucheza kama beki wa kati na hata beki wa kulia unampa Arteta chaguo bora, hususan katika kipindi hiki ambacho kikosi kinakabiliwa na majeraha ya William Saliba na Jurrien Timber. Ingawa beki huyo hatashiriki mchezo wa ufunguzi wa ligi dhidi ya Coventry City, anatarajiwa kufanya debut yake ya kwanza katika mchezo ujao dhidi ya klabu yake ya zamani, Aston Villa, pale Villa Park mnamo Agosti 31.
Hatima ya Julian Alvarez
Wakati Arsenal ikiimarisha ulinzi, jitihada zao za kutafuta mshambuliaji mpya zimekutana na kizingiti. Ingawa kumekuwa na taarifa za Atletico Madrid kukubali kumuuza Julian Alvarez kwa Arsenal, mchezaji huyo mwenyewe bado ana msimamo mwingine.
Ripoti kutoka vyombo mbalimbali vya habari, zikithibitishwa na Graeme Bailey wa TEAMtalk, zinaeleza kuwa Alvarez hataki kujiunga na Arsenal. Mshambuliaji huyo wa Argentina ana ndoto moja tu: kujiunga na Barcelona.
“Julian Alvarez bado hayuko tayari kufikiria uhamisho kwenda Arsenal kwani Barcelona wanabaki na nia ya kujaribu kukamilisha dili kwa mshambuliaji huyo wa Atletico Madrid kabla ya dirisha la usajili kufungwa,” ilisema sehemu ya taarifa hiyo.
Inaonekana hali ya Alvarez ndani ya Atletico Madrid imekuwa ngumu, lakini nia yake ya kutaka kuvaa jezi ya miamba hiyo ya Catalonia inaendelea kuwa kikwazo kwa Arsenal wanaotaka kumpata ili kuimarisha safu yao ya ushambuliaji.