Arsenal yajipanga kutoa mshahara mnono kumnasa Vinicius Junior kutoka Real Madrid
Arsenal yataka kufanya kweli kwa Vinicius Junior
Klabu ya Arsenal inaripotiwa kuweka mipango kabambe ya kumsajili mshambuliaji wa Real Madrid, Vinicius Junior, katika dirisha hili la usajili. Kocha Mikel Arteta anaonekana kuvutiwa sana na uwezo wa nyota huyo wa kimataifa wa Brazil na amemweka kama chaguo lake kuu la kuimarisha safu ya ushambuliaji.
Taarifa kutoka vyombo mbalimbali nchini Uingereza, zikiwemo The Athletic na BBC Sport, zinaeleza kuwa ndani ya klabu hiyo ya London wamekubaliana kuanza mchakato wa kutafuta uwezekano wa kumpata mchezaji huyo. Ingawa bado hawajafanya mawasiliano rasmi na Real Madrid, Arsenal wameonyesha nia ya dhati ya kufanikisha dili hilo ambalo litakuwa ni kubwa zaidi katika historia ya klabu hiyo.
Arteta amezama kwenye penzi la Vinicius
Baada ya kuondoka kwa Leandro Trossard aliyeelekea Besiktas, Arsenal wamekuwa wakitafuta mbadala mahiri wa kucheza pembeni, hasa upande wa kushoto. Ingawa tayari wameshamsajili Christos Tzolis kutoka Club Brugge, inaonekana Arteta bado hajaridhika na anataka mtu mwenye uwezo mkubwa wa kubadilisha matokeo ya mchezo.
Ripoti zinaonyesha kuwa baada ya kukosa saini ya Morgan Rogers aliyetua Chelsea, Arteta amehamishia nguvu zake zote kwa Vinicius. Chanzo cha karibu na klabu hiyo kimesema:
“Ingawa kuna wachezaji wengine wanaotazamwa na klabu, Arteta amevutiwa sana na wazo la kumsajili Vinicius kiasi kwamba ndani ya Arsenal, anatazamwa kama chaguo namba moja.”
Rekodi ya mishahara iko hatarini
Ili kufanikisha usajili huu wa kihistoria, Arsenal wapo tayari kuweka rekodi mpya ya mshahara klabuni hapo. Vinicius, ambaye mkataba wake na Real Madrid unamalizika mwaka 2027, kwa sasa anapokea kiasi cha pauni 400,000 kwa wiki.
Ili kumshawishi nyota huyo kuondoka Hispania na kujiunga na washindi hao wa Ligi Kuu ya England, Arsenal wamejipanga kuongeza dau hilo ili kuvunja rekodi ya mishahara iliyopo sasa klabuni. Aidha, inatarajiwa kuwa gharama ya usajili wake inaweza kuvunja rekodi ya ada kubwa zaidi ya uhamisho nchini Uingereza, rekodi inayoshikiliwa kwa sasa na Alexander Isak.
Changamoto za usajili
Licha ya nia ya Arsenal, changamoto kubwa bado inabaki kwa upande wa Real Madrid. Vinicius bado anaonekana kutaka kusalia katika dimba la Santiago Bernabeu na anatazamia kusaini mkataba mpya. Hata hivyo, kutokana na mkataba wake kuelekea ukingoni, Real Madrid watalazimika kufanya maamuzi magumu iwapo mchezaji huyo hatakuwa tayari kuongeza muda wa kubaki klabuni hapo, jambo ambalo linaweza kuwapa mwanya Arsenal kuingilia kati.