Arsenal yafunga milango ya kumsajili Kenan Yildiz, Gabriel Martinelli mbioni kuondoka
Arsenal yafuta mpango wa kumsajili Yildiz
Ndoto za mashabiki wa Arsenal kumuona nyota wa Juventus, Kenan Yildiz, akitua katika Uwanja wa Emirates zimefikia mwisho. Ripoti za muda mrefu zilizokuwa zikimuhusisha mshambuliaji huyo kijana na miamba hiyo ya London zimezimwa rasmi kufuatia hali halisi ya mambo.
Mtaalamu wa masuala ya uhamisho wa wachezaji, Fabrizio Romano, ameweka mambo wazi kwa kusisitiza kuwa Juventus hawakuwa na nia yoyote ya kumuuza nyota huyo, na sasa hali imekuwa mbaya zaidi baada ya Yildiz kupata jeraha kubwa la mguu katika mchezo wa ufunguzi wa Serie A, ambalo linaweza kuhitaji upasuaji.
Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisema:
“Kuna jeraha kwa Kenan Yildiz. Kama bado kuna hadithi za Yildiz na Arsenal… kila mara nimekuwa nikiweka wazi, kama unataka kujua kama Arsenal wanampenda Yildiz? Bila shaka wanampenda, nani asiyempenda Yildiz? Lakini huu siyo mpango wa wiki hii, hii ni hadithi ya kuanzia Aprili, Mei, Juni. Arsenal siku zote walimthamini Yildiz. Lakini walijua kuwa Juventus hawamuuzi mchezaji huyo. Hiyo ndiyo basi, mwisho wa hadithi tangu Mei, kwa hiyo hakuna nafasi. Na sasa Yildiz ameumia, atakuwa nje kwa muda, kwa hiyo sahau kuhusu hilo.”
Gabriel Martinelli katika mlango wa kutokea
Wakati mpango wa Yildiz ukifutika, hali ni tofauti kwa mshambuliaji Gabriel Martinelli. Inaonekana Arsenal wameamua kuendelea na mchakato wa kumuuza mshambuliaji huyo wa Brazil kuelekea klabu ya Al-Hilal ya Saudi Arabia.
Taarifa za hivi karibuni zinaonyesha kuwa Arsenal wamekubali kupunguza kiasi cha ada ya uhamisho kutoka ile ya awali ya pauni milioni 60. Sasa, klabu hiyo ipo tayari kumuuza Martinelli kwa dau linalokadiriwa kuwa kati ya pauni milioni 50 hadi 55.
Jambo muhimu ni kwamba mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 25 amefungua milango ya kuhamia Mashariki ya Kati, jambo ambalo linafanya dili hilo kupiga hatua kubwa kuelekea kukamilika. Kwa sasa, Arsenal wanaonekana kuelekeza nguvu zao zaidi katika maeneo mengine ya usajili, huku uwezekano wa kumsajili mbadala wa Martinelli ukionekana kuahirishwa hadi dirisha lijalo la usajili.
Wakati huu wote, Arsenal wamekuwa wakijaribu kuimarisha safu yao ya ushambuliaji, huku jina la Julian Alvarez likitajwa kuwa lengo kubwa zaidi kwa klabu hiyo katika siku za mwisho za dirisha hili la usajili.