Arsenal yaweka kipengele maalum kwenye dili la mkopo la Ethan Nwaneri kwenda Dortmund
Uamuzi wa kimkakati wa Arsenal kwa chipukizi Nwaneri
Klabu ya Arsenal imethibitisha kuwa na mpango wa muda mrefu kwa kinda wao, Ethan Nwaneri, baada ya kumuachia ajiunge na Borussia Dortmund kwa mkopo. Uhamisho huu unaelezwa kuwa na kipengele maalum ambacho kiliwekwa na mabingwa hao wa London ili kuhakikisha wanakua na udhibiti wa hatma ya mchezaji huyo.
Taarifa kutoka kwa mtaalamu wa usajili, Fabrizio Romano, zinaeleza kuwa dili hilo ni la mkopo wa kawaida ambao hauna kipengele cha Dortmund kumnunua jumla mchezaji huyo mwisho wa msimu. Hii inaonyesha kuwa Arsenal bado inamhitaji Nwaneri katika mipango yake ya baadaye.
Kipengele cha ‘Recall’ ni muhimu
Katika mazungumzo hayo, ilibainika kuwa Arsenal ilisisitiza kuingiza kipengele cha kumrejesha mchezaji (recall clause) kama sharti kuu la makubaliano hayo. Bila sharti hilo, inaonekana klabu ya Arsenal haikuwa tayari kumwachia kinda huyo kwenda Ujerumani.
“Borussia Dortmund wamekubali kuingiza kipengele maalum cha kumrejesha mchezaji kwenye mkataba na Arsenal. Bila sharti hilo, dili hilo lisingetimia,” alieleza Romano.
Kipengele hicho kina maelekezo ya kifedha pia. Iwapo Arsenal wataamua kumrejesha Nwaneri katika dirisha la usajili la Januari, Borussia Dortmund watarejeshewa ada ya mkopo waliyoilipa, huku wao wakiwa wamegharamia tu mishahara ya mchezaji huyo kwa kipindi alichokuwepo huko.
Matumaini ya Niko Kovac kwa Nwaneri
Kwa upande wake, kocha wa Borussia Dortmund, Niko Kovac, amemwagia sifa lukuki kinda huyo, akiamini kuwa atakuwa na mchango mkubwa katika kikosi chake msimu huu.
Kovac aliliambia vyombo vya habari: “Tulikuwa tukimtafuta mchezaji wa aina yake kwenye nafasi hiyo; mtu mwenye uwezo wa kupambana mmoja dhidi ya mmoja, mwenye kasi na mbunifu wa kuwatoka mabeki. Nwaneri ni mchezaji mwenye kipaji kikubwa.”
Nwaneri, ambaye amewahi kuandika historia ya kuwa mchezaji mdogo zaidi kuwahi kucheza Ligi Kuu ya England, anatarajiwa kupata uzoefu zaidi nchini Ujerumani baada ya msimu uliopita kutokuwa na wakati mzuri wa kucheza mara kwa mara akiwa Marseille.