Aurelien Tchouameni yuko tayari kujiunga na Man Utd kwa sharti moja
Hatua mpya katika usajili wa kiungo wa Real Madrid
Manchester United wanaonekana kuongeza kasi katika kusaka mrithi wa Casemiro kwenye safu yao ya kiungo, huku taarifa za hivi punde zikionyesha kuwa kiungo wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni, yuko tayari kujiunga na klabu hiyo ya Old Trafford.
Licha ya awali kuonekana kuwa ni ngumu kumsajili mchezaji huyo wa timu ya taifa ya Ufaransa, ripoti kutoka kwa mwandishi Dean Jones zinaeleza kuwa dili hilo linawezekana kabisa msimu huu. Tchouameni anafahamu vyema kuhusu juhudi za Manchester United kumshawishi, na inaonekana amefungua mlango wa kutua England.
Sharti moja la Tchouameni
Mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 26 ameweka wazi kuwa yuko tayari kuondoka Real Madrid na kutua United, lakini kwa sharti moja muhimu: uongozi wa Real Madrid uwe umemthibitishia kuwa hana nafasi tena katika mipango yao ya siku zijazo kwenye Uwanja wa Santiago Bernabeu.
Ingawa Real Madrid haijawahi kuwa klabu ya kukurupuka kuuza mastaa wake, hali ya kikosi chao kwa sasa chini ya kocha Jose Mourinho inaweza kubadilika. Baada ya kusajili nyota kama Denzel Dumfries, Ibrahima Konate, Marc Cucurella na Bernardo Silva, klabu hiyo inahitaji kupunguza idadi ya wachezaji na kupata fedha ili kuweka uwiano sawa, jambo ambalo linafungua mlango wa kuuzwa kwa mastaa wakubwa.
Dau la kuvunja rekodi kutoka INEOS
Manchester United chini ya uongozi wa INEOS wanaonekana nia yao ni kuimarisha eneo la kiungo baada ya Casemiro kuondoka kujiunga na Inter Miami na Manuel Ugarte kupata jeraha kubwa la goti (ACL) wakati wa michuano ya Kombe la Dunia. Ripoti za Mundo Deportivo zinaeleza kuwa United wamejipanga kuweka mezani dau la zaidi ya Euro milioni 100 (takriban pauni milioni 85) ili kuhakikisha wananasa huduma ya kiungo huyo.
Kiasi hicho cha pesa kinalenga kuishawishi Real Madrid kuruhusu mauzo hayo ya haraka, huku United wakimwona Tchouameni kama mchezaji sahihi kabisa wa kuziba pengo la Casemiro katikati ya uwanja.
Focus ipo kwenye Kombe la Dunia
Pamoja na tetesi hizi zote, mchezaji mwenyewe bado hajachukua uamuzi wa mwisho kwa sasa. Kipaumbele chake kikubwa ni kuisaidia timu ya taifa ya Ufaransa kufanya vizuri kwenye michuano ya Kombe la Dunia.
“Tchouameni hatatoa uamuzi wowote wakati huu akijikita kwenye kuisaidia timu yake kushinda Kombe la Dunia,” ilieleza ripoti hiyo.
Ufaransa sasa wanajiandaa kwa mchezo wa robo fainali dhidi ya Morocco utakaopigwa usiku wa Alhamisi, na mashabiki wa Manchester United watakuwa wakifuatilia kwa karibu maendeleo ya kiungo huyo kabla ya mazungumzo ya kina kuanza rasmi kati ya klabu hizo mbili.