Bacary Sagna: Leny Yoro angefanya vizuri zaidi Arsenal kuliko Manchester United
Changamoto ya Leny Yoro Old Trafford
Beki wa zamani wa Arsenal, Bacary Sagna, ametoa mtazamo wake kuhusu mwenendo wa beki kijana Leny Yoro tangu alipojiunga na Manchester United. Yoro, ambaye alinaswa kwa ada ya paundi milioni 52 kutoka Lille, amekuwa akipata wakati mgumu kupata nafasi ya kudumu katika kikosi cha kwanza cha United chini ya makocha tofauti, wakiwemo Ruben Amorim na sasa Michael Carrick.
Tangu ajiunge na miamba hiyo ya Old Trafford, mchezaji huyo mwenye umri wa miaka 20 amekuwa akipambana kuingia kwenye kikosi cha kwanza, huku akionekana kupitwa na wazoefu Harry Maguire na Lisandro Martinez. Katika msimu huu, amepata nafasi ya kucheza mara mbili tu kama mchezaji wa akiba kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.
‘Timu ilikuwa inaumwa’
Sagna, ambaye alikuwa beki tegemeo jijini London, anaamini kuwa kiwango cha Yoro kimeathiriwa kwa kiasi kikubwa na hali ya Manchester United kama klabu. Kwa mujibu wa Sagna, mchezaji mchanga anahitaji mazingira tulivu na yenye utaratibu mzuri ili kuonesha uwezo wake kamili.
“Yeye ni mchezaji mzuri, lakini alijiunga na timu iliyokuwa inaumwa. Wakati anasajiliwa, hali haikuwa nzuri ndani ya klabu hiyo. Ni vigumu kwa mchezaji kung’ara binafsi wakati timu nzima inapata shida. Ikiwa timu nzima ina matatizo, ni rahisi na wewe kuambukizwa matatizo hayo na kujikuta kwenye wakati mgumu kama beki,” Sagna aliliambia Action Network.
Arsenal ingekuwa chaguo tofauti
Sagna anaamini kuwa kama Yoro angechagua kujiunga na Arsenal mwaka 2024, hali ingekuwa tofauti kabisa. Anasema kuwa mazingira ya sasa ya Arsenal, ambayo yamekuwa na mwendelezo mzuri wa matokeo na mfumo uliotulia, yangempa kijana huyo nafasi kubwa ya kukua na kuonesha kipaji chake.
“Kama angekuja Arsenal na kuona timu inang’ara, pengine naye angekuwa anang’ara. Sio suala la ubora wa mchezaji pekee, bali ni namna timu inavyofanya kazi wakati huo. Ni matumaini yangu United watarejea kwenye mstari na Yoro atapata msimu mzuri kwa sababu ni mchezaji wa kiwango cha juu,” aliongeza Sagna.
Nafasi yake uwanjani
Sio tu suala la timu, bali hata matumizi ya mchezaji huyo yamezua mijadala. Legend wa Manchester United, Gary Neville, amekosoa kitendo cha Carrick kumtumia Yoro kama beki wa kulia wakati mwingine, akisisitiza kuwa mchezaji huyo anapaswa kucheza kama beki wa kati pekee.
“Sidhani kama anaelewa vyema kucheza beki wa kulia, jambo ambalo ni la kawaida kwa mabeki wengi wa kati. Tunapaswa kuacha kumtumia hapo na kufikiria yeye ni beki wa kulia,” Neville alionya kupitia The Overlap.