Barcelona waanza kuhoji nia ya Julian Alvarez kujiunga nao
Barcelona yajihisi kutumiwa
Klabu ya Barcelona imeanza kuingia na mashaka juu ya nia halisi ya mshambuliaji wa Atletico Madrid, Julian Alvarez, katika dirisha hili la usajili. Inaripotiwa kuwa viongozi wa miamba hiyo ya Catalan wanaanza kuhisi kuwa mchezaji huyo anaitumia klabu yao kama chambo ili kuongeza thamani yake katika mazungumzo na klabu nyingine.
Alvarez amekuwa akihusishwa kwa karibu na mpango wa kutaka kuondoka Atletico Madrid, huku kukiwa na taarifa kuwa anapendelea kujiunga na Barcelona ili kupata changamoto mpya na kushindania mataji makubwa. Hata hivyo, hali ya mambo kati ya Atletico na Barcelona inaelezwa kuwa ni ya kiushindani na ya mvutano mkubwa, hali inayofanya dili hilo kuwa gumu.
Mchezo wa maslahi binafsi?
Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, anaripotiwa kutaka uwazi kuhusu suala hili. Flick hafurahishwi na wazo la klabu yake kutumia muda mwingi na nguvu za kifedha kufuatilia mchezaji ambaye huenda hana nia ya dhati ya kujiunga na klabu hiyo, bali anaitumia kama njia ya kushinikiza maboresho ya mkataba wake.
Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa wawakilishi wa Alvarez wanatambua kuwa Arsenal nao wanammezea mate mshambuliaji huyo. Kwa kutajwa kwa Barcelona kama chaguo jingine, inawapa nafasi nzuri ya kuishinikiza Arsenal kuongeza dau la mshahara, au hata kuilazimisha Atletico Madrid kumpa mkataba bora zaidi ili abaki.
“Flick hataki Barça itumie majira yote ya joto kuhifadhi fedha kwa ajili ya dili ambalo huenda halikuwahi kuwa na nafasi ya kufanikiwa. Ndio maana amemuagiza Deco (Mkurugenzi wa Michezo) kujua nia ya kweli ya Mwargentina huyo haraka iwezekanavyo,” ilieleza taarifa hiyo.
Arsenal wanapashwa kulipa?
Kwa upande wake, Arsenal wanaendelea kufuatilia hali hiyo kwa ukaribu sana. Baada ya kukosa saini ya Morgan Rogers, kocha Mikel Arteta anaonekana kuhitaji mshambuliaji mwenye kiwango cha juu ili kuimarisha safu yake ya ushambuliaji.
Gwiji wa Manchester United, Paul Scholes, amewashauri Arsenal wasipoteze muda na badala yake watoe pesa yoyote inayohitajika ili kumpata Alvarez.
“Kama Atletico Madrid wanataka pauni milioni 100, klabu yoyote kubwa inapaswa kwenda na kumnasa. Hakuna mjadala hapo. Sioni kama kuna washambuliaji wengi wa daraja la juu walio katika soko kwa sasa,” alisema Scholes kupitia podcast ya The Good, The Bad & The Football.
Suala hili linabaki kuwa tete kwani Atletico Madrid wameonyesha nia ya kutomuuza mchezaji huyo kwa mpinzani wao wa ligi, Barcelona, huku wakionekana kuwa na utayari wa kusikiliza ofa kutoka nje ya Hispania, hasa Arsenal.