Bradley Barcola kwenye rada za Liverpool na Arsenal
Barcola kuondoka PSG?
Klabu za Liverpool na Arsenal zinaendelea kufuatilia kwa ukaribu hali ya mshambuliaji wa Paris Saint-Germain (PSG), Bradley Barcola. Taarifa za hivi punde kutoka kwa mchambuzi wa soka David Ornstein zinaeleza kuwa mchezaji huyo wa kimataifa wa Ufaransa yuko tayari kufikiria changamoto mpya nje ya Ufaransa ili kupata nafasi ya kudumu ya kucheza kwenye kikosi cha kwanza.
Kwa sasa, PSG inakabiliwa na ushindani mkali wa namba katika safu ya ushambuliaji kutokana na uwepo wa nyota kama Khvicha Kvaratskhelia na Desire Doue. Vilevile, klabu hiyo inatajwa kuwa kwenye harakati za kuwasajili wachezaji kama Yan Diomande na Maghnes Akliouche, jambo ambalo linaweza kumfanya Barcola kupoteza nafasi yake zaidi kwenye kikosi cha kwanza cha kocha wao.
Liverpool na Arsenal ziko tayari
Ornstein amethibitisha kuwa Liverpool ni miongoni mwa klabu zinazomhitaji sana mshambuliaji huyo, ingawa Arsenal pia imekuwa ikitajwa mara kwa mara kama mshindani mkuu wa saini yake.
“Liverpool wanampenda sana Bradley Barcola. PSG wangependa kumuweka, lakini wapo ‘realist’ (wanajua hali halisi). Ana miaka miwili tu iliyobaki kwenye mkataba wake. Yeye si mchezaji wa kuanza mara kwa mara, na anataka kuwa hivyo, hivyo nahisi angekuwa wazi kwa uhamisho ikiwa fursa sahihi itajitokeza,” alisema Ornstein kupitia The Athletic FC Podcast.
Changamoto ya nafasi uwanjani
Licha ya kuvutiwa na uwezo wake, kuna mjadala mkubwa kuhusu nafasi anayocheza Barcola. Mfaransa huyo mara nyingi anacheza upande wa kushoto wa uwanja, wakati ambapo Liverpool wanatafuta mchezaji wa kuziba pengo la Mohamed Salah upande wa kulia. Hii inaleta swali kama mchezaji huyo atakuwa tayari kubadili mchezo wake ili kuendana na mahitaji ya Anfield.
Bei ya uhamisho
Inaelezwa kuwa PSG haitakubali kumuuwa mchezaji huyo kwa bei chee. Kwa kuzingatia soko la sasa ambapo ada za usajili zimepanda kwa kiasi kikubwa, inakadiriwa kuwa mchezaji yeyote atakayetaka kumnunua Barcola atalazimika kutoa zaidi ya pauni milioni 116. Hata hivyo, Ornstein alisisitiza kuwa kwa sasa mazungumzo hayajafika hatua za juu.
Kwa sasa, Barcola yupo kwenye majukumu ya timu yake ya taifa ya Ufaransa katika michuano ya Kombe la Dunia, na uongozi wa PSG umeamua kutoingilia umakini wake. Inatarajiwa kuwa hatima ya mchezaji huyo itajulikana zaidi mara baada ya mashindano hayo kumalizika.