Jamie Carragher aibua hofu Liverpool, Alexis Mac Allister apata mtetezi
Hofu ya Carragher kuhusu usajili wa Liverpool
Gwiji wa Liverpool, Jamie Carragher, ameeleza wasiwasi wake mkubwa kuhusu mwelekeo wa klabu hiyo katika kipindi cha usajili. Ingawa Liverpool wameanza msimu wa 2026/27 kwa matokeo ya mchanganyiko, ushindi wao wa 2-1 dhidi ya Atletico Madrid kwenye mchezo wa ufunguzi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya umeacha maswali mengi kuliko majibu kwa baadhi ya wadau.
Carragher anaamini kuwa Liverpool wamepoteza dira katika kuimarisha kikosi, kwa kuamua kusajili majina makubwa badala ya kutafuta wachezaji wanaoweza kuendana na mfumo wa timu. Akizungumza na CBS Sports, Carragher alisema:
“Inatia hofu kidogo kwangu kwa Liverpool, na jambo hili lilitokea msimu wa joto uliopita. Inaonekana kama tumekuwa klabu inayochagua majina makubwa badala ya kufikiria wachezaji hao wataingia vipi kwenye mfumo wa timu. Kwa sasa, Liverpool wana majina makubwa na vipaji binafsi, lakini sijaona jinsi kila kitu kitakavyoungana na kufanya kazi kama timu moja.”
Mac Allister na malalamiko ya mkataba
Wakati Carragher akizungumzia muundo wa kikosi, kiungo Alexis Mac Allister amekuwa gumzo baada ya kufunga bao la ushindi dhidi ya Atletico Madrid, huku akiwa amekasirishwa na uongozi wa Liverpool kwa kutompa ofa ya mkataba mpya.
Mchezaji huyo wa Argentina, ambaye mkataba wake wa sasa unaisha mwaka 2028, amekuwa akipata presha kutokana na kiwango chake cha msimu uliopita. Hata hivyo, beki wa zamani wa Liverpool, Stephen Warnock, anaamini kuwa tatizo si Mac Allister, bali ni mfumo wa timu.
”Mfumo wa timu haujakaa sawa”
Warnock anaitaja timu ya sasa ya Liverpool kama iliyo katika hali ya “kuyumba” (dysfunctional), hali ambayo inamfanya mchezaji mwenye ubora kama Mac Allister kushindwa kuonyesha makali yake halisi uwanjani.
“Sidhani kama Mac Allister anahitaji kuthibitisha umuhimu wake Liverpool, kila mtu anajua ubora alionao. Anahitaji kuwekwa kwenye mfumo sahihi ili mambo yaende. Kwa sasa, mfumo wa Liverpool haujakaa sawa vizuri, ingawa unaanza kuimarika kidogo. Mac Allister atafanya vizuri zaidi kadiri timu itakavyokuwa bora,” alisema Warnock.
Warnock ameongeza kuwa ni jambo la kupendeza kuona Mac Allister akijibu presha ya mkataba kwa kiwango bora uwanjani, akisisitiza kuwa kama ataendelea kuonyesha kiwango kizuri msimu huu, klabu italazimika kumfikiria vyema kuhusu mkataba wake.