Carragher Aionya Liverpool Kuhusu Uteuzi wa Iraola: "Ni Hatari Kujaribu Kumuiga Klopp"
Mlinzi wa zamani na gwiji wa Liverpool, Jamie Carragher, ameibuka na kuweka wazi wasiwasi wake juu ya uteuzi wa kocha mpya wa klabu hiyo, Andoni Iraola. Carragher amebainisha vigezo vitatu vikuu ambavyo kocha yeyote anayeajiriwa na klabu kubwa Ulaya anapaswa kuwa navyo, na kudai kuwa kocha huyo wa zamani wa Bournemouth “anakidhi kigezo kimoja tu” kati ya hivyo.
Liverpool walifanya maamuzi magumu ya kumfuta kazi Arne Slot mwishoni mwa mwezi uliopita baada ya timu hiyo kumaliza katika nafasi ya tano kwenye msimamo wa Ligi Kuu ya Uingereza (Premier League). Matokeo na kiwango cha timu hiyo vilionekana kushuka kwa kasi, hasa ikilinganishwa na msimu wa 2024/25 ambapo walitwaa ubingwa wa ligi hiyo.
Baada ya taarifa rasmi ya Liverpool siku ya Alhamisi kuthibitisha kuwa Iraola ndiye atakayechukua mikoba ya kuinoa timu hiyo, kocha huyo raia wa Basque alieleza furaha yake kubwa ya kujiunga na klabu hiyo aliyoiita “ya kipekee.”
Akizungumza kuhusu changamoto hiyo mpya, Iraola alisema:
“Nimefurahi sana, nina shauku kubwa kweli kweli. Kila mtu anaijua Liverpool, unajua ni klabu kubwa sana, moja ya klabu kubwa zaidi duniani. Lakini nikiwa hapa ndani na kuanza kuielewa klabu hii kwa ukaribu zaidi, daima nimekuwa nikiamini kuwa ni klabu ya kipekee.”
“Huitaji mambo mengi ili uvutiwe na Liverpool. Liverpool ni Liverpool tu. Lakini bila shaka, mazingira ya hapa, mashabiki, klabu yenyewe, wachezaji, na fursa ya mimi kufundisha wachezaji wa kiwango cha juu na kupigania mataji—naona hakuna kitu chenye kuvutia zaidi ya hiki. Ni vigumu kupata nafasi kama hii, hivyo nina shauku kubwa kuanza kazi.”
Kuwasili kwa Iraola kumepokelewa kwa hisia chanya na mashabiki wengi wa Liverpool, ambao wana matumaini kuwa ataweza kuleta soka la kuvutia na la kushambulia ambalo Bournemouth walikuwa wakilicheza chini yake pale Anfield.
Mtego wa Kumuiga Jurgen Klopp
Hata hivyo, Carragher anaamini kuwa kufanya maamuzi ya kuajiri kocha kwa matumaini kuwa ataiga mtindo wa soka uliomfanya Jurgen Klopp kuwa gwiji na kipenzi cha mashabiki Anfield ni “uamuzi wa hatari.”
Katika makala yake kwenye gazeti la Telegraph, Carragher aliandika:
“Vigezo vikuu vya kufundisha moja ya timu bora zaidi Ulaya vinapaswa kujikita kwenye kile ambacho mgombea ameshinda, amefundisha katika kiwango gani, na kwa mtindo gani wa uchezaji. Iraola anakidhi kigezo kimoja tu kati ya hivyo. Hoja yake kubwa ya kujiunga na Liverpool ni kwamba kikosi chake cha Bournemouth kilicheza soka linalofanana na jinsi Klopp alivyopenda timu yake icheze.”
“Inashangaza pia kuona jinsi taarifa zote zinazotoka ndani ya klabu zinavyoonyesha nia ya dhati ya kutaka mtu ambaye uongozi unamchukulia kama aliye karibu zaidi na mtindo wa Mjerumani huyo (Klopp) kuliko Slot. Kila uteuzi wa kocha una riski yake, lakini kuwapima makocha wa baadaye wa Liverpool kwa kuangalia tu kama wanaendana na dhana ya soka la ‘heavy-metal’ ni jambo la hatari.”
Carragher aliongeza kuwa kupunguza mafanikio ya Klopp na kumuona kama kocha aliyefanikiwa kwa sababu tu ya mbinu za kukaba kwa nguvu (high-pressing) na soka la kushambulia ni makosa makubwa yanayopotosha uhalisia wa ukubwa wa kocha huyo na sababu zilizomfanya yeye na Liverpool kuwa pacha waliopendana.
Changamoto Mpya kwa Iraola
Mchambuzi huyo alihitimisha kwa kueleza kuwa hatua hii ni kubwa mno na imekuja mapema sana kwa Iraola, ambaye bado hajapata uzoefu wa kutosha katika michuano mikubwa ya Ulaya.
“Wakati Iraola alipokuwa akihusishwa sana na Chelsea, mtazamo wangu ulikuwa kwamba bado ilikuwa mapema sana kwake. Alihitaji kwanza kujiunga na klabu inayoshiriki michuano ya Ulaya ili azoee changamoto ya kucheza mechi tatu kwa wiki kama maandalizi ya hatua inayofuata. Badala yake, sasa atakutana na changamoto kubwa pale Liverpool ambazo hajawahi kukutana nazo maishani mwake wa ukocha.”
Kazi kubwa sasa inabaki kwa Iraola kudhibitisha kuwa Carragher amekosea, huku akijaribu kuirudisha Liverpool kwenye reli ya ushindani wa mataji makubwa msimu ujao.