Skip to content

Carragher atoa rai kuhusu hatima ya Michael Carrick Manchester United

SokaNews
Updated: Published: Ijumaa, 25 Septemba 2026 · 2 min read
manchesterunited michaelcarrick jamiecarragher premierleague ineos sokalauingereza
Carragher atoa rai kuhusu hatima ya Michael Carrick Manchester United

Uamuzi wa kumfuta Carrick unaonekana kuwa wa haraka

Jamie Carragher, gwiji wa zamani wa Liverpool na mchambuzi wa soka, amesisitiza kuwa itakuwa ni uamuzi wa ‘kijinga’ kwa Manchester United kumfuta kazi kocha Michael Carrick katika kipindi hiki. Licha ya timu hiyo kuanza msimu kwa kusuasua, Carragher anaamini kuwa ni mapema mno kufanya maamuzi magumu.

Carrick alipewa mkataba wa kudumu mwezi Mei baada ya kuionyesha vizuri timu hiyo akiwa kama kocha wa mpito. Katika kipindi hicho, aliisaidia United kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye msimamo wa Premier League, huku akipata ushindi muhimu dhidi ya timu kubwa kama Manchester City, Arsenal, Tottenham, Chelsea na Liverpool.

Changamoto za msimu huu

Hata hivyo, hali imekuwa tofauti msimu huu ambapo United imeshinda mchezo mmoja tu kati ya mitano iliyopita. Presha imeongezeka baada ya kufungwa kwenye dabi ya Manchester na kutolewa katika Kombe la Ligi na Brighton baada ya kuongoza kwa mabao mawili. Pia, walinusurika kichapo dhidi ya Fulham kupitia bao la bahati nasibu dakika za lala salama.

Akizungumza kwenye kipindi cha The Overlap Fan Debate, Carragher alisema:

“Nadhani itakuwa ni ujinga kumfuta kazi Michael Carrick sasa. Sioni kama yeye ni kocha wa muda mrefu wa Manchester United. Nahisi kama anafanya kazi ya kuivusha klabu katika kipindi kigumu ili baadaye akabidhi kijiti kwa mtu mwingine.”

Carragher aliongeza kuwa haoni sababu ya msingi ya kufanya mabadiliko ya kocha sasa au wakati wa mapumziko ya kimataifa, akisisitiza kuwa klabu inapaswa kuwa na subira.

Lawama kwa uongozi

Wakati presha ikizidi kuelekezwa kwa Carrick, wapo wanaohisi kuwa tatizo si yeye pekee. Mick Brown, ofisa wa zamani wa United, amesema kuwa uongozi wa klabu unapaswa kubeba sehemu kubwa ya lawama kwa kushindwa kumpa kocha huyo kikosi chenye ushindani.

“Kuna presha kubwa kwa Michael Carrick kuleta matokeo, lakini hawezi kubeba lawama peke yake kwa sababu uongozi umeshindwa kumpa sapoti anayohitaji. Anafanya kazi na kile alichonacho,” alisema Brown.

Brown alibainisha kuwa safu ya ulinzi ya United haina ubora wa kutosha na kuna sintofahamu kubwa katika eneo la ushambuliaji na viungo, mambo ambayo uongozi haukuyashughulikia kikamilifu kwenye dirisha la usajili. Kwa sasa, Carrick anaonekana kama mtu anayewajibishwa kwa makosa ambayo hayapo mikononi mwake.