Chelsea yafunga dili la kihistoria kwa kinda wa Marekani, Garnacho atua Aston Villa
Chelsea wanasaka vipaji vya baadaye
Baada ya kuweka rekodi ya uhamisho kwa kumnasa Morgan Rogers kwa kitita cha pauni milioni 117, klabu ya Chelsea imeendelea kuonyesha dhamira yao ya kujenga kikosi cha kutisha kwa sasa na baadaye. Safari hii, The Blues wamefanikiwa kumpata kinda mwenye kipaji kikubwa kutoka nchini Marekani, Benji Flowers.
Ingawa ana umri wa miaka 15 tu, usajili wa Flowers umetajwa kuwa wa kihistoria kutokana na mchakato wake na thamani iliyowekezwa. Kinda huyu anayemudu kucheza kama winga wa kushoto, amesaini mkataba na klabu yake ya sasa ya FC Dallas, huku kukikiwa na makubaliano rasmi kwamba atajiunga na Chelsea pindi tu atakapofikisha umri wa miaka 18.
Ujumbe wa ‘Here We Go’ kwa Flowers
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, tayari amethibitisha dili hilo kwa kauli yake maarufu ya ‘here we go’. Kwa mujibu wa ripoti, Chelsea itagharimika kiasi cha dola milioni 10 kwa ajili ya kinda huyu, ikijumuisha ada ya awali ya dola milioni 3 na nyingine milioni 7 kama nyongeza kulingana na mafanikio yake.
Chelsea wamekubaliana kila kitu kumsajili winga mwenye kipaji kutoka Marekani, Benji Flowers, kwa ajili ya akademi yao. Atajiunga na timu hiyo pindi tu atakapofikisha miaka 18, - Fabrizio Romano.
Wachambuzi wanaeleza kuwa Chelsea imepata upinzani mkali kutoka kwa klabu nyingine za Ulaya na Mexico zilizokuwa zikimwania kinda huyu, lakini ushawishi wa The Blues umefanikiwa kumpata mchezaji huyo ambaye tayari amewahi kutembelea England kukamilisha taratibu za awali.
Alejandro Garnacho rasmi Aston Villa
Wakati Chelsea ikiimarisha akademi yake, mshambuliaji Alejandro Garnacho amekamilisha rasmi safari yake ya kuelekea klabu ya Aston Villa. Mchezaji huyu amejiunga na kikosi cha Unai Emery kwa mkopo wenye kipengele cha lazima cha kununuliwa moja kwa moja.
Ripoti zinaeleza kuwa mkataba huo una vipengele ambavyo ni rahisi kufikiwa ili uhamisho huo uwe wa kudumu. Ben Jacobs, mwandishi wa habari za michezo, amebainisha kuwa mkataba huo unategemea idadi ya michezo ambayo mchezaji atacheza.
Inakadiriwa kuwa Chelsea itapata kiasi cha euro milioni 50 (pauni milioni 43), ambazo zinajumuisha ada ya mkopo na kiasi kitakacholipwa baada ya kukamilisha masharti hayo ya kudumu. Garnacho tayari ameshapokea jezi namba 17 atakayoitumia katika uwanja wa Villa Park msimu huu.