Cole Palmer afunguka kuhusu kuachwa katika kikosi cha England kwenye Kombe la Dunia
Palmer aelezea hisia zake baada ya kutemwa
Kiungo mshambuliaji wa Chelsea, Cole Palmer, hatimaye amevunja ukimya kuhusu kuachwa kwake katika kikosi cha timu ya taifa ya England kinachoshiriki michuano ya Kombe la Dunia mwaka huu. Uamuzi wa kocha Thomas Tuchel kumwacha mchezaji huyo umekuwa gumzo kubwa miongoni mwa wachambuzi na mashabiki wa soka.
Palmer, ambaye msimu huu hakuwa katika kiwango chake bora kutokana na changamoto za majeruhi, alijikuta nje ya kikosi kilichosafiri kwenda kwenye michuano hiyo, huku England ikiamua kutumia wachezaji wengine kama Jude Bellingham, Morgan Rogers na Eberechi Eze katika safu ya kiungo ushambuliaji.
Anakubaliana na maoni ya wachambuzi
Wachambuzi mashuhuri kama Wayne Rooney na Jamie Carragher ni miongoni mwa waliokosoa uamuzi wa Tuchel, wakidai kuwa England ilikuwa na uhitaji wa ubunifu wa Palmer na Phil Foden katika michezo migumu ambapo timu ilihitaji mchezaji mwenye uwezo wa kucheza kwenye nafasi finyu.
Akizungumza na gazeti la The Times, Palmer alikiri kuwa inatia moyo kuona watu wanamthamini, lakini anabaki na msimamo wake wa kuheshimu uamuzi wa kocha.
“Bila shaka ni kitu kizuri kuona watu wananikumbuka, lakini ukweli ni kwamba mimi sipo huko. Najua kitu ambacho ningeweza kukiongeza kwenye timu, kitu tofauti na kile ambacho kocha amekichagua. Lakini kama nilivyosema awali, siwezi kubadilisha maamuzi hayo na nawatakia kila la kheri wenzangu.”
Maisha nje ya Kombe la Dunia
Pamoja na maumivu ya kukosa michuano hiyo mikubwa duniani, Palmer anajaribu kutazama upande wa pili wa shilingi. Kwa mara ya kwanza tangu aanze kucheza soka la ushindani, amepata fursa ya kupata mapumziko marefu ya majira ya joto.
“Nimekuwa nikitazama mechi kila ninapopata nafasi. Nafurahia mapumziko yangu na kufanya mambo tofauti, lakini nikitulia nyumbani na mechi ikiwa inaendelea, huwa naitazama,” aliongeza Palmer.
Alipoulizwa kama anajuta kukosa nafasi hiyo, mchezaji huyo alijibu kwa uwazi: “Bila shaka, kila mchezaji wa soka anatamani kuwa kwenye Kombe la Dunia. Ni uamuzi ambao siwezi kuubadilisha na ulikuwa mgumu, kwa sababu yoyote ile. Hivyo, najaribu tu kufurahia mapumziko haya ya kiangazi, likizo yangu ya kwanza niliyopata tangu nianze soka.”
Kwa sasa, England inaendelea na kampeni zake kuelekea hatua ya 16 bora, ambapo inatarajiwa kupambana na wenyeji Mexico katika uwanja wa Azteca, mchezo ambao unatarajiwa kuwa na upinzani mkali.