Cristian Romero kuondoka Tottenham: Atletico Madrid yapiga hodi, Arsenal wajitoa
Hatima ya Romero yafahamika
Safari ya beki wa kimataifa wa Argentina, Cristian Romero ndani ya klabu ya Tottenham Hotspur inaelekea ukingoni. Baada ya uvumi mwingi kuzunguka mustakabali wake katika dirisha hili la usajili, taarifa za karibuni zinaonyesha kuwa mchezaji huyo amefanya maamuzi ya kuelekea nchini Uhispania kujiunga na Atletico Madrid.
Awali, kuliibuka taarifa kuwa Arsenal walikuwa miongoni mwa klabu zilizokuwa zikimnyemelea beki huyo ili kuziba pengo la William Saliba aliyepata majeraha. Hata hivyo, imebainika kuwa kuna makubaliano ya kimyakimya kati ya Arsenal na Tottenham kwamba uhamisho wa aina hiyo hauwezi kutokea, kutokana na ushindani mkubwa uliopo kati ya timu hizo mbili za London.
Kwa nini Arsenal walijitoa?
Mchambuzi wa masuala ya soka na aliyewahi kuwa mtaalamu wa kusaka vipaji Ligi Kuu ya England, Mick Brown, ameweka wazi kuwa usajili wa Romero kwenda Emirates haukuwa na mashiko.
“Ingekuwa jambo la kushangaza sana kumuona Romero akihamia Arsenal. Sidhani kama jambo hilo lilikuwa na uhalisia wowote. Tottenham hawako tayari kumuuza mchezaji wao kwa mpinzani wao mkuu, na hata Arsenal wana hofu juu ya jinsi ingekavyoonekana mbele ya mashabiki wao,” alisema Brown.
Brown aliongeza kuwa Arsenal inaonekana kuelekeza nguvu zao kwenye malengo mengine ya usajili badala ya kumng’ang’ania beki huyo ambaye msimu uliopita alikabiliwa na changamoto za majeraha mara kwa mara.
Atletico Madrid ndio chaguo la ‘Cuti’
Wakati Arsenal wakijitoa, klabu ya Atletico Madrid inayoongozwa na Diego ‘Cholo’ Simeone imefanikiwa kumpata beki huyo. Mwandishi wa habari za michezo, Nicolo Schira, amethibitisha kuwa mazungumzo hayo yapo katika hatua za mwisho.
Inaelezwa kuwa Romero amekubali mkataba wa hadi mwaka 2030, huku kukiwa na chaguo la kuongeza msimu mmoja zaidi. Mchezaji huyo mwenyewe anatajwa kuwashukuru wadau mbalimbali, ikiwemo Inter Milan, Barcelona na Arsenal kwa nia yao ya kumsajili, lakini ameamua kuwa kuelekea jijini Madrid ndio chaguo lake sahihi.
Ushawishi wa Diego Simeone umekuwa nguzo kuu ya uamuzi huu, kwani kocha huyo amekuwa akimfuatilia Romero kwa misimu kadhaa iliyopita. Kwa sasa, Tottenham wanaendelea na mipango yao baada ya kusajili mabeki wengine kama Jan Paul van Hecke na Marcos Senesi kuziba nafasi ya Margentina huyo.