Cristiano Ronaldo: Ureno haikushinda chochote bila mimi
Mwisho wa safari ya Ronaldo kwenye Kombe la Dunia
Safari ya Cristiano Ronaldo katika Kombe la Dunia imefika tamati kwa namna ya kusikitisha baada ya Ureno kupoteza kwa bao 1-0 dhidi ya Hispania katika hatua ya 16 bora. Bao hilo lililofungwa na Mikel Merino dakika za mwisho za mchezo liliiacha Ureno bila majibu na kuondoa ndoto ya nyota huyo mwenye umri wa miaka 41 kutwaa taji hilo kubwa kabla ya kustaafu.
Akizungumza na waandishi wa habari baada ya mchezo huo, Ronaldo hakuonyesha haraka ya kutangaza kustaafu soka la kimataifa, akisisitiza kuwa anahitaji muda wa kutafakari na kuwa na familia yake kwanza.
“Nimesikitika kuondoka kwenye Kombe la Dunia kwa namna hii. Nimejituma kwa kila hali. Nimefanya vyema na naondoka nikiwa na dhamiri safi. Ilikuwa Kombe langu la mwisho la Dunia, ndiyo, lakini sasa nitakuwa na muda wa kutafakari. Sitafanya maamuzi ya haraka,” alisema Ronaldo.
Kiburi cha mafanikio
Licha ya kufungwa, Ronaldo hakusita kujivunia mchango wake mkubwa kwa timu ya taifa ya Ureno tangu aanze kuitumikia. Alisisitiza kuwa yeye ndiye aliyeleta mapinduzi ya ushindi katika soka la nchi hiyo.
“Nimeshinda mataji matatu kwa ajili ya Ureno; kabla ya Cristiano Ronaldo, Ureno haikuwa imeshinda taji hata moja,” aliongeza staa huyo wa Al-Nassr.
Alikumbusha pia kuwa taji la Euro 2016 kwake lina uzito sawa na Kombe la Dunia, akiliona kama mafanikio makubwa zaidi kwa timu hiyo ya taifa.
Kuondoka kwa Roberto Martinez
Mechi hiyo pia ilikuwa ya mwisho kwa kocha wa Ureno, Roberto Martinez, ambaye alithibitisha kuondoka kwake mara baada ya mchezo huo. Ronaldo alimwagia sifa kocha huyo kwa kazi kubwa aliyoifanya.
“Nilifurahia kufanya kazi naye. Ni kocha mzuri, mtu mwenye utu, na kile alichokifanya kwa Ureno kinastahili pongezi. Nataka kumshukuru na kumtakia kila la kheri,” alisema Ronaldo.
Kwa upande wake, Martinez alisema kuwa mkataba wake umeisha na ni wakati wa uongozi wa shirikisho la soka la Ureno kutafuta mbadala wake. Alisema anaondoka akiwa na fahari ya kupewa nafasi ya kuiongoza timu hiyo na kujihisi kama mmoja wa raia wa Ureno kutokana na mapokezi aliyopata.