DILI LA ALVAREZ: Barcelona Wamtengea Mshahara wa Kufuru, Arsenal Waingia Wasiwasi
Mshambuliaji wa kimataifa wa Argentina, Julian Alvarez, amelipua bomu la usajili baada ya kutangaza hadharani nia yake ya kutaka kuondoka Atletico Madrid msimu huu wa kiangazi. Hatua hiyo imezindua vita kali ya kuwania saini yake kati ya miamba ya soka ya Hispania, Barcelona, na vigogo wa Ligi Kuu ya Uingereza, Arsenal.
Alvarez alitoa kauli hiyo mara baada ya mchezo wa Kombe la Dunia wa mwaka 2026 kati ya Argentina na Austria, ambapo alikiri kuwa mustakabali wake upo mbali na Atletico Madrid.
Julian Alvarez Afunguka Kuhusu Mustakabali Wake
Katika kile kinachoonekana kama shinikizo kwa uongozi wa Atletico Madrid, mshambuliaji huyo wa zamani wa Manchester City aliweka wazi kuwa ameshazungumza na wahusika na suluhisho bora ni yeye kuondoka.
Alvarez alinukuliwa na BBC Sport akisema:
“Niliongea na watu wa [Atletico] niliopaswa kuongea nao, na jambo bora zaidi kwa kila mtu ni mimi kuhama. Nataka kutimiza ndoto yangu. Haya si wakati mzuri wa kulizungumzia hili, lakini pia siwezi kulificha. Najaribu kuwa mtu mkweli kila wakati.”
Barcelona Ndio Ndoto Kubwa ya Alvarez
Mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, amefichua kuwa ndoto kubwa ya mchezaji huyo ni kujiunga na miamba wa Katalunya, Barcelona. Romano ameeleza kuwa Alvarez tayari amekataa ofa kutoka kwa Paris Saint-Germain (PSG) na Arsenal kwa sababu anataka kwenda Camp Nou tu.
Kulingana na Romano, PSG walijaribu kumshawishi lakini mchezaji huyo akawajibu: “Asanteni, lakini nataka kwenda Barcelona.” Arsenal nao walipata jibu lile lile walipojaribu kufanya mawasiliano na kambi ya mchezaji huyo.
Hata hivyo, Atletico Madrid hawako tayari kumuuza Alvarez kwenda kwa washindani wao wa karibu wa La Liga (Barcelona) na wangependelea kumuuza nje ya Hispania ikiwa atalazimika kuondoka. Hali hii inaiweka Arsenal kwenye nafasi nzuri endapo dili la Barca litagonga mwamba.
Arsenal Wagoma Kufanya Kufuru ya Fedha
Licha ya Arsenal kummezea mate mshambuliaji huyo tingu msimu uliopita, ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa viongozi vya juu wa klabu hiyo ya London Kaskazini wana hofu ya kulipa kiasi kikubwa cha fedha.
Mwandishi wa habari za michezo, Diego Torres Romano, amefichua kuwa baadhi ya viongozi wenye ushawishi mkubwa pale Arsenal wametahadharisha klabu hiyo dhidi ya kulipa zaidi ya euro milioni 100 (pauni milioni 86.2) kama ada ya usajili wa Alvarez.
Pia, kuna tofauti kubwa ya kimaslahi. Barcelona imeripotiwa kumtengenezea Alvarez ofa ya mshahara wa euro milioni 18 safi kwa mwaka (net), kiasi kinacholingana na kile anachopokea kinda Lamine Yamal. Kwa upande wao, Arsenal wapo tayari kutoa euro milioni 12 pekee safi kwa mwaka, wakiona kulipa zaidi ya hapo ni hatari kubwa kifedha.
Je, Milango Bado Iko Wazi kwa Arsenal?
Licha ya upendeleo wa Alvarez kwenda Barcelona, taarifa kutoka kwa vyanzo vya ndani vya Arsenal zinasema mchezaji huyo hajafunga kabisa milango kwa miamba hao wa London.
Inasemekana kuwa Alvarez yuko tayari kujiunga na Arsenal chini ya kocha Mikel Arteta endapo tu ndoto yake ya kwenda Barcelona itashindikana kutokana na ugumu wa kifedha wa klabu hiyo au msimamo wa Atletico kutotaka kuwauzia wapinzani wao wa nyumbani.
Pia, ripoti zinasema Atletico Madrid wana nia ya kumsajili mshambuliaji Viktor Gyokeres, jambo linaloweza kufanya klabu hizo mbili kufanya biashara kirahisi katika siku zijazo ikiwa mazungumzo rasmi yataanza.