Djed Spence hatihati kuikosa Mexico, Thomas Tuchel anafikiria mbadala
Changamoto ya beki wa kulia inaendelea
Timu ya taifa ya England inakabiliwa na wakati mgumu katika safu yake ya ulinzi kuelekea mchezo ujao wa Kombe la Dunia dhidi ya Mexico. Habari mpya kutoka kambi ya ‘Three Lions’ zinaashiria kuwa beki wao wa kulia, Djed Spence, huenda asishiriki mchezo huo kutokana na kusumbuliwa na jeraha.
Hii ni sehemu ya mfululizo wa changamoto ambazo England imekuwa ikikutana nazo katika nafasi hiyo ya beki wa kulia tangu kuanza kwa mashindano haya. Awali, Tino Livramento alitolewa nje kabla ya mashindano kuanza, huku Reece James akicheza mechi mbili pekee kabla ya naye kuingia katika orodha ya majeruhi.
Uamuzi mgumu kwa Tuchel
Ripoti kutoka kwa mwandishi wa Sky Sports, Rob Dorsett, zinaeleza kuwa beki huyo wa Tottenham yupo katika hali ya kusikilizia maumivu, jambo linalomfanya kocha Thomas Tuchel kulazimika kutafuta mbadala wa dharura.
“Tunajua ana matatizo katika nafasi ya beki wa kulia, tunajua Declan Rice yuko fiti. Swali ni je, atacheza nafasi yake ya kawaida katikati ya uwanja au atacheza kama beki wa kulia?” alieleza Dorsett.
Kwa sasa, chaguo la kocha Tuchel linaonekana kuwa ni kati ya Jarell Quansah, ambaye amerejea mazoezini baada ya kupona, au kumpanga kiungo Declan Rice katika nafasi hiyo ya pembeni.
Hofu dhidi ya Mexico
Kutokuwa na beki wa asili katika nafasi ya kulia kunaleta hofu kubwa kwa England, hasa wakizingatia ubora wa mshambuliaji wa Mexico, Julian Quinones. Quinones, anayekipiga katika klabu ya Al-Qadsiah, amekuwa katika kiwango bora sana katika mashindano haya, akiwa amefunga mabao matatu na kutoa pasi moja ya bao hadi sasa.
Uwezo wake wa kupambana upande wa kushoto dhidi ya beki ambaye si wa asili katika nafasi hiyo, unaweza kuwa mtihani mkubwa kwa safu ya ulinzi ya England. Tuchel atalazimika kufanya uamuzi wa busara ili kuhakikisha hawapati matokeo mabaya dhidi ya timu hiyo iliyoonyesha makali yake dhidi ya Ecuador.