Skip to content

Eddie Howe anukia kuchukua mikoba ya Thomas Tuchel England

SokaNews
Updated: Published: Alhamisi, 16 Julai 2026 · 2 min read
england thomastuchel eddiehowe newcastleunited kombeladunia sokalaulaya
Eddie Howe anukia kuchukua mikoba ya Thomas Tuchel England

Shinikizo la kumtimua Tuchel lapaa

Mustakabali wa Thomas Tuchel kama kocha mkuu wa timu ya taifa ya England uko mashakani baada ya kuondolewa kwenye Kombe la Dunia na Argentina. England ilitolewa katika hatua ya nusu fainali kwa kufungwa mabao 2-1, matokeo ambayo yameibua gumzo kubwa miongoni mwa wadau wa soka nchini humo.

Licha ya England kutangulia kupata bao kupitia kwa Anthony Gordon na kuonekana kuanza vyema mchezo, mabadiliko ya kiufundi yaliyofanywa na Tuchel katika kipindi cha pili yameonekana kuigharimu timu hiyo. Kocha huyo alikosolewa kwa kufanya mabadiliko ya kujilinda ambayo yaliwapa nafasi Argentina kurudi mchezoni na kupindua meza.

Eddie Howe yuko tayari

Katika hali ya kushangaza, taarifa zinasema kuwa kocha wa Newcastle United, Eddie Howe, anatajwa kuwa tayari kuachana na klabu hiyo ili kuchukua mikoba ya kuinoa England iwapo Tuchel atapoteza kibarua chake.

Ripoti zinaeleza kuwa ndani ya kambi ya England, baadhi ya wachezaji wameanza kueleza mashaka yao juu ya mbinu za Tuchel, wakidai kuwa kocha huyo alipanga timu kwa lengo la kutopoteza badala ya kupambana ili kushinda. Howe, ambaye amekuwa na changamoto katika dirisha la usajili akiwa na Newcastle, anaonekana kuwa na nia ya dhati ya kupata changamoto mpya katika ngazi ya timu ya taifa.

Lawama nzito kwa Tuchel

Kiwango cha hasira dhidi ya Tuchel kimefikia hatua ya baadhi ya wachambuzi nchini England kudai kuwa kocha huyo anapaswa kuondoka mara moja. Jamie O’Hara, mchezaji wa zamani wa Tottenham, hakuwa na maneno ya kuficha alipozungumzia mchezo huo.

“Alitugharimu Kombe la Dunia. Tulikuwa mbele kwa bao 1-0, tulitakiwa kuwa na ujasiri. Hii ndiyo sababu tulimleta kwa ajili ya wakati huu mgumu. Tulimtoa Gareth Southgate kwa sababu hatukuwa na ujasiri, lakini leo tumefanya kilekile.”

O’Hara aliongeza kwa hasira:

“Tumeondolewa kwa aibu. Anapaswa kufutwa kazi, aondoke haraka iwezekanavyo.”

Ingawa Tuchel aliongeza mkataba wake wa kuinoa England hadi mwaka 2028 kabla ya mashindano haya kuanza, shinikizo hili jipya kutoka kwa mashabiki, wachambuzi, na taarifa za ndani kuhusu nia ya Howe, linaweza kuilazimisha FA kufanya uamuzi mgumu hivi karibuni.