Eduardo Camavinga aondoka Real Madrid? Fabrizio Romano afunguka
Hatma ya Camavinga Bernabeu
Mustakabali wa kiungo wa Real Madrid, Eduardo Camavinga, umezua mjadala mkubwa katika dirisha hili la usajili kufuatia taarifa zinazomhusisha na kutaka kuhamia mabingwa wa England, Manchester City.
Ripoti za hivi karibuni kutoka nchini Hispania zilidai kuwa tayari kumekuwa na mazungumzo ya moja kwa moja kati ya klabu hizo mbili. Inasemekana kuwa kocha mpya wa Madrid, Jose Mourinho, yupo tayari kumwachia kiungo huyo ili kupata fedha za kusajili wachezaji wengine anaohitaji kuimarisha kikosi chake, hasa katika eneo la kiungo na ulinzi wa kati.
Msimamo wa Camavinga
Licha ya minong’ono hiyo, mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, ameweka wazi kuwa mchezaji huyo hana mpango wowote wa kuondoka Santiago Bernabeu.
Katika ufafanuzi wake, Romano alisisitiza kuwa Camavinga amewaeleza mawakala wake nia yake ya dhati ya kubaki na kupambana kwa ajili ya nafasi yake kwenye kikosi cha Mourinho.
“Eduardo Camavinga ana nia ya wazi na ameshaieleza mawakala wake. Anataka kubaki Real Madrid. Anataka kuendelea kuchezea klabu hii na kuwa sehemu ya kikosi msimu ujao. Hataki kuondoka baada ya msimu mbaya,” alisema Romano.
Je, Real Madrid wanamuuza?
Romano aliongeza kuwa hali ni tofauti kati ya klabu na mchezaji. Wakati Camavinga akitamani kubaki, Real Madrid kwa upande wao wako tayari kumsikiliza yeyote mwenye ofa mezani kwa ajili ya kumsajili nyota huyo wa Ufaransa.
“Real Madrid wako wazi kumuuza Camavinga. Ikitokea ofa nzuri, watafungua mlango. Lakini tatizo ni kwamba mchezaji mwenyewe hataki kuondoka,” aliongeza mchambuzi huyo.
Kuhusu Manchester City, Romano alifafanua kuwa kwa sasa hakuna mazungumzo ya kina au ofa rasmi iliyowasilishwa. City wanajua tu kuwa Madrid wanaweza kumuuza mchezaji huyo na wanaangalia uwezekano wa kuongeza kiungo mwingine, lakini hakuna hatua kubwa iliyochukuliwa hadi sasa.
Kwa sasa, Camavinga anaonekana kuwa na nia ya kujituma zaidi ili kujisahihisha baada ya msimu uliopita ambao uligubikwa na changamoto kadhaa, ikiwemo kadi nyekundu, majeruhi, na kushindwa kucheza Kombe la Dunia.