Erling Haaland afunguka kuhusu mustakabali wake Man City ikishushwa daraja
Haaland hataki kucheza daraja la pili
Mustakabali wa straika matata wa Manchester City, Erling Haaland, umeendelea kuwa gumzo baada ya taarifa mpya kuibuka kuwa staa huyo hana nia ya kuendelea kuichezea timu hiyo endapo itashushwa daraja. Hatua hii inakuja kufuatia klabu hiyo ya Etihad kukabiliwa na tuhuma nzito 115 za kuvunja kanuni za matumizi ya fedha (FFP) katika Ligi Kuu ya England.
Ripoti kutoka Hispania zinaeleza kuwa wawakilishi wa Haaland tayari wamefanya mazungumzo na mabingwa wa La Liga, FC Barcelona, ili kupima upepo na kujua hatua wanazoweza kuchukua iwapo hali itakuwa mbaya kwa City.
Hakuna vipengele vya kuondoka bure
Licha ya kuwepo kwa uvumi mwingi juu ya uwepo wa vipengele (release clauses) kwenye mikataba ya wachezaji wa City ambavyo vingewawezesha kuondoka bure endapo timu itashushwa daraja, vyanzo vya ndani ya klabu hiyo vimekanusha vikali suala hilo. Inafahamika kuwa hakuna mchezaji yeyote, ikiwemo Haaland, mwenye kipengele cha aina hiyo kwenye mkataba wake.
“Majibu ambayo Barcelona wanayahitaji yako wazi: Mnorway huyu hana nia yoyote ya kucheza katika daraja la pili (Second Division),” ilieleza ripoti kutoka nchini Hispania.
Hata hivyo, kutokuwepo kwa kipengele hicho hakumaanishi kuwa Haaland atashindwa kuondoka. Ikiwa klabu itashushwa daraja, itakuwa vigumu kwa City kuwazuia wachezaji nyota kama yeye, na hali hiyo ingeifanya klabu hiyo kuwa na msimamo dhaifu wa mazungumzo, jambo ambalo linaweza kufungua mlango kwa Barcelona kumnasa mshambuliaji huyo kwa dau la kuridhisha.
Barcelona wanajipanga mapema
Barcelona inaonekana kutaka kuwa mstari wa mbele kuhakikisha wanapata huduma ya Haaland iwapo fursa itajitokeza mnamo mwaka 2027. Mkurugenzi wa michezo wa klabu hiyo ya Catalonia tayari amekutana na wawakilishi wa mchezaji huyo kwa takriban saa moja ili kuelewa msimamo wake.
Ingawa mkataba wa Haaland na Manchester City unatarajiwa kudumu hadi 2034, mabadiliko makubwa yatakayotokana na maamuzi ya kesi ya FFP yanatarajiwa kubadili sura ya soka nchini England na barani Ulaya kwa ujumla. Kwa sasa, mashabiki wa City wanasubiri kwa hamu hatima ya klabu yao, huku kukiwa na hofu ya kupokonywa mataji, kupigwa faini, au hata kufukuzwa kabisa kwenye ligi ikiwa watapatikana na hatia ya kuvunja kanuni hizo.