Everton wameweka msimamo wao: Jarrad Branthwaite hauzwi kwenda Liverpool
Everton wamekataa mazungumzo
Matumaini ya Liverpool kumsajili beki wa Everton, Jarrad Branthwaite, yamegonga mwamba baada ya klabu hiyo ya Goodison Park kuweka wazi kuwa mchezaji huyo hauzwi. Ripoti zimekuwa zikihusisha beki huyo wa kimataifa wa Uingereza na mpango wa kutua Anfield kama mbadala wa muda mrefu wa nahodha Virgil van Dijk.
Hata hivyo, taarifa kutoka ndani ya Everton zinasema kuwa mabosi wa klabu hiyo hawana mpango wowote wa kumruhusu beki huyo mwenye umri wa miaka 24 kuondoka, hasa kuelekea kwa mahasimu wao wakubwa wa Merseyside. Branthwaite anaonekana kuwa mhimili muhimu katika safu ya ulinzi ya kocha David Moyes.
Mkataba wa muda mrefu unawapa jeuri Everton
Uamuzi wa Everton kuendelea kumng’ang’ania beki huyo unachochewa na mkataba wake ambao unatarajiwa kumalizika mwaka 2030. Tangu Moyes aliporudi klabuni hapo Januari 2025, alisisitiza kuwa kumhifadhi Branthwaite ni moja ya vipaumbele vyake vikubwa, jambo ambalo uongozi wa klabu umelitimiza kwa kumpa mkataba mpya.
“Everton hawana shinikizo la kumuuza mchezaji huyo. Branthwaite anaonekana kama mchezaji muhimu sana kikosini na hayupo kwenye soko kwa ajili ya mauzo,” taarifa ilieleza.
Liverpool wanatafuta mrithi wa Van Dijk
Kwa upande wa Liverpool, mpango wa kutafuta beki mpya umekuwa kipaumbele kutokana na umri wa Virgil van Dijk kusogea. Mick Brown, aliyekuwa mkuu wa skauti wa Manchester United, ameeleza kuwa Liverpool wanajua fika umuhimu wa kujiimarisha sehemu hiyo ya ulinzi.
Brown alisema: “Liverpool wana shida na hali ya mkataba wa Van Dijk. Ana umri wa miaka 35 sasa na atafikisha 36 wakati mkataba wake utakapomalizika mwakani. Ni wazi wanafanya kazi nyuma ya pazia kutafuta mrithi wake, na Branthwaite ni mmoja wa wachezaji wanaowavutia sana.”
Licha ya Liverpool kuvutiwa na uwezo wa beki huyo wa kushoto, Everton wamesimama kidete. Inasemekana kuwa itahitaji ofa ya kishindo isiyo ya kawaida ili kuwashawishi Everton kubadili mawazo yao, jambo ambalo linaonekana kuwa gumu kwa sasa kutokana na ushindani mkali wa klabu hizi mbili.