Skip to content

Chama cha Soka cha England (FA) chaweka msimamo kuhusu hatima ya Thomas Tuchel

SokaNews
Updated: Published: Alhamisi, 16 Julai 2026 · 2 min read
thomastuchel england fa kombeladunia argentina fabrizioromano
Chama cha Soka cha England (FA) chaweka msimamo kuhusu hatima ya Thomas Tuchel

FA yaweka msimamo kuhusu Thomas Tuchel

Chama cha Soka cha England (FA) kimeondoa hofu ya mashabiki wa timu hiyo ya taifa kwa kuthibitisha kuwa hakina nia ya kumtimua kocha Thomas Tuchel, licha ya kipigo cha kusikitisha dhidi ya Argentina katika mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia.

England ilikuwa ikiongoza kupitia goli la Anthony Gordon, lakini mambo yalienda kombo kipindi cha pili baada ya kocha Tuchel kufanya mabadiliko ya kiulinzi kwa kumuingiza Ezri Konsa na kucheza na mabeki watano. Uamuzi huo uliiruhusu Argentina kutawala mchezo, kusawazisha kupitia kwa Enzo Fernandez, na hatimaye Lautaro Martinez kufunga goli la ushindi katika dakika za lala salama.

Uamuzi wa FA kubaki na Tuchel

Mchambuzi maarufu Fabrizio Romano, kupitia chaneli yake ya YouTube, amefafanua kuwa ndani ya FA kuna imani kubwa kwa Tuchel licha ya ukosoaji mkubwa uliojitokeza mitandaoni.

“Ujumbe kutoka kwa watu wa karibu na shirikisho la soka la England baada ya mchezo dhidi ya Argentina ni kwamba, licha ya kukatishwa tamaa na kutolewa nusu fainali na ukosoaji wa mashabiki, FA wanataka kuendelea na Tuchel. Wanataka abaki na kuwa sehemu ya mradi wa muda mrefu wa timu ya taifa ya England,” alisema Romano.

Romano ameongeza kuwa FA inapanga kukutana na Tuchel katika siku za hivi karibuni ili kuweka bayana dhamira yao ya kuendelea naye, huku uamuzi wa mwisho ukitarajiwa kubaki kwa kocha mwenyewe kama atakuwa tayari kuendelea na majukumu hayo.

Upinzani mkali dhidi ya Tuchel

Hata hivyo, si kila mtu anayekubaliana na msimamo wa FA. Mchezaji wa zamani wa Tottenham, Jamie O’Hara, amekuwa miongoni mwa watu walioonyesha kukerwa na mbinu za Tuchel, akidai kuwa kocha huyo ndiye aliyesababisha England kupoteza nafasi hiyo ya kuingia fainali.

Akiongea kwa hisia kali, O’Hara alisema:

“Tuchel ametugharimu Kombe la Dunia! Tulikuwa tunaongoza 1-0, tulitakiwa kuwa jasiri. Tulimleta yeye kwa ajili ya nyakati kama hizi. Ni uamuzi mbaya, ni fedheha. Anapaswa kufukuzwa kazi, aondoke!”

Licha ya presha hizo kutoka kwa wachambuzi na sehemu ya mashabiki, inaonekana uongozi wa FA bado una imani na mradi wa Tuchel, wakilenga kujenga timu kwa ajili ya mafanikio ya baadaye badala ya kuchukua hatua za haraka kufuatia matokeo hayo ya nusu fainali.