Fabrizio Romano afafanua kuhusu Arsenal na Bradley Barcola
Arsenal hawajafanya mawasiliano kwa Barcola
Kufuatia kupoteza fursa ya kumsajili Morgan Rogers aliyeelekea Chelsea kwa kiasi cha Pauni milioni 117, mashabiki wa Arsenal wamekuwa na shauku kubwa ya kujua nani atakuwa mbadala wake. Jina la winga wa Paris Saint-Germain, Bradley Barcola, limekuwa likitajwa mara kwa mara kama mlengwa mkuu wa The Gunners.
Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya uhamisho barani Ulaya, Fabrizio Romano, amewakata maini mashabiki hao kwa kusema kuwa hakuna hatua zozote za dhati ambazo Arsenal wamezichukua kumsaka mchezaji huyo.
“Mashabiki wengi wa Arsenal wamekuwa wakiniuliza kama sasa klabu yao inaenda kumsaka Barcola kwa nguvu. Guys, ufahamu wangu ni kwamba kufikia sasa Arsenal hawajafanya mawasiliano yoyote ya dhati. Mazungumzo kati ya Arsenal na Barcola bado ni baridi sana,” alisema Romano kupitia chaneli yake ya YouTube.
Liverpool bado wanashikilia hatamu
Wakati Arsenal wakiwa bado hawajapiga hatua, hali ni tofauti kwa Liverpool. Romano amethibitisha kuwa klabu hiyo ya Anfield bado ina nia kubwa ya kumnasa staa huyo wa Ufaransa.
“Liverpool wanabaki kuwa makini sana na wapo tayari kumsajili Barcola. Ninasisitiza kuwa uhamisho huu bado ni uwezekano mkubwa, ingawa kila kitu kitategemea kiasi cha pesa ambacho PSG watahitaji, kwani wanataka ada kubwa,” aliongeza Romano.
Pigo kwa Arsenal kuhusu Yan Diomande
Sio Barcola tu, Arsenal pia wamekutana na changamoto katika juhudi zao za kuimarisha nafasi ya winga. Ripoti zinaeleza kuwa walijaribu kuulizia uwezekano wa kumsajili Yan Diomande kutoka RB Leipzig, lakini waligonga mwamba.
Diomande tayari ameshamalizana na Paris Saint-Germain kuhusu maslahi binafsi, na klabu hizo mbili ziko kwenye mazungumzo ya mwisho kukamilisha dili hilo. Arsenal walijaribu kupenya katikati ili kuona kama kuna nafasi ya kuingilia kati, lakini walichelewa.
Nini kinafuata baada ya kukosa Rogers?
Kupoteza nafasi ya kumsajili Morgan Rogers ni pigo kubwa kwa Mikel Arteta, ambaye alikuwa akimhitaji sana mchezaji huyo tangu miezi ya kwanza ya mwaka huu. Rogers, ambaye anaitumikia England kwenye Kombe la Dunia, anatarajiwa kufanyiwa vipimo vya afya jijini London Jumatatu ijayo ili kukamilisha uhamisho wake kwenda Chelsea.
Ingawa Arsenal wameshakubaliana na Club Brugge kuhusu usajili wa Christos Tzolis, ni wazi kuwa klabu hiyo itahitaji kufanya kazi ya ziada katika dirisha hili ili kuziba mapengo yaliyopo kwenye kikosi chao.