Fabrizio Romano aondoa utata wa Viktor Gyokeres kujiunga na Barcelona
Hakuna mazungumzo kati ya Barcelona na Gyokeres
Mtaalamu wa masuala ya uhamisho wa wachezaji barani Ulaya, Fabrizio Romano, amewatoa hofu mashabiki wa Arsenal kufuatia uvumi uliokuwa ukisambaa kuhusu mshambuliaji wao, Viktor Gyokeres.
Kulikuwa na taarifa nyingi zikidai kuwa miamba ya soka nchini Hispania, Barcelona, walikuwa wanajiandaa kufanya msako wa kumsajili mshambuliaji huyo wa kimataifa wa Sweden katika kipindi hiki cha dirisha la usajili. Hata hivyo, Romano amesisitiza kuwa hakuna ukweli wowote katika madai hayo.
Kupitia channel yake ya YouTube, Romano alifafanua:
“Kumeibuka taarifa nyingi nchini Hispania katika saa 24 zilizopita zikidai kuwa Viktor Gyokeres anaweza kuwa mtu sahihi kwa Barcelona ikiwa watashindwa kumpata Julian Alvarez. Hakuna uthibitisho wowote wa operesheni inayoendelea kumhusu Gyokeres. Hakuna mazungumzo, hakuna majadiliano yanayoendelea kwa sasa.”
Arsenal wana imani na Gyokeres
Licha ya mshambuliaji huyo kupata changamoto ya kufunga mabao mara kwa mara katika msimu wake wa kwanza ndani ya uwanja wa Emirates, ambapo alifunga mabao 21 katika michezo 55, Arsenal inaonekana bado inamuamini sana mchezaji huyo.
Romano aliongeza kuwa kocha wa Arsenal, Mikel Arteta, bado anauona umuhimu wa staa huyo katika kikosi chake kwa ajili ya msimu ujao.
“Kwa sasa, hisia ndani ya Arsenal ni kwamba Viktor Gyokeres atabaki. Mikel Arteta ana furaha naye na anaamini kuwa Arsenal inahitaji mchezaji wa aina yake ndani ya kikosi. Klabu ina imani kubwa kuwa msimu wa pili wa Gyokeres kwenye Ligi Kuu ya England utakuwa tofauti na utaonyesha kiwango bora zaidi,” aliongeza Romano.
Maoni ya Shay Given kuhusu safu ya ushambuliaji
Ingawa klabu ina imani na Gyokeres, mjadala kuhusu uwezo wa Arsenal kuimarisha safu yake ya ushambuliaji bado unaendelea. Kipa wa zamani wa Newcastle United na Manchester City, Shay Given, hivi karibuni alitoa maoni yake akidai kuwa Arsenal inahitaji mshambuliaji mwingine mwenye uwezo wa kumaliza nafasi.
Given alisema: “Viktor Gyokeres alifanya vizuri msimu uliopita, lakini bado naona kama wanataka kushinda mataji mengi, wanahitaji mtu pale mbele ambaye anahitaji nafasi moja tu kufunga bao, siyo nafasi tatu au nne kwa mchezo mmoja.”
Kwa sasa, inaonekana Arsenal hawana haraka ya kufanya mabadiliko katika safu hiyo ya ushambuliaji, huku Gyokeres akitarajiwa kuendelea kupambania nafasi yake ndani ya kikosi cha Arteta.