Fabrizio Romano atoa ufafanuzi kuhusu Arsenal kumtaka Victor Osimhen
Hali ya mambo baada ya Alvarez kukataa ofa ya Arsenal
Mambo yameonekana kuwa magumu kwa Mikel Arteta katika harakati zake za kutafuta mshambuliaji mpya kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Julian Alvarez, ambaye alikuwa ndiye chaguo namba moja la Arsenal, ametoa uamuzi wa moja kwa moja kwa kocha huyo wa ‘The Gunners’ kuwa hataki kujiunga na klabu hiyo.
Awali, klabu ya Atletico Madrid ilionyesha utayari wa kumuuza mshambuliaji huyo kwa kiasi kikubwa cha pesa ambacho kingeweka rekodi ya usajili ghali zaidi nchini Uingereza, takriban paundi milioni 128. Hata hivyo, dili hilo limekwama kutokana na mchezaji mwenyewe kutokuwa na nia ya kuhamia Emirates.
Mwandishi nguli wa masuala ya usajili, David Ornstein, alithibitisha hali hiyo kwa kusema:
“Kwa sasa, nafasi ya yeye kujiunga na Arsenal ni ndogo sana kwa sababu moyo wake ulikuwa unaelekea Barcelona. Atletico wamefunga mlango kwa Barcelona, na Arsenal walikuwa tayari kufikia makubaliano, lakini mchezaji hajaonyesha dalili zozote za kutaka kujiunga nao. Amemwambia Mikel Arteta moja kwa moja kuwa hataki kuja.”
Ingawa Ornstein aliongeza kuwa mambo yanaweza kubadilika katika soka, kwa sasa matumaini ya kumnasa Alvarez yanaonekana kupotea.
Romano aondoa utata wa Victor Osimhen
Kufuatia kufeli kwa dili la Alvarez, mashabiki wengi wa Arsenal wamekuwa wakihoji kama klabu hiyo itageukia kwa staa wa Nigeria, Victor Osimhen, ambaye kwa sasa anachezea Galatasaray. Hata hivyo, mtaalamu wa usajili, Fabrizio Romano, ametoa tamko kali la kufunga mjadala huo.
Kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano amesisitiza kuwa hakuna ukweli wowote kuhusu tetesi hizo zinazowahusisha Arsenal na Osimhen.
“Si kweli wakuu. Arsenal hawajawahi kuanzisha mazungumzo yoyote kwa ajili ya Osimhen. Sababu ni moja tu: Osimhen haendi popote. Yeye ni sehemu ya mkakati wa Galatasaray na hakuwa kwenye soko wala hakuwahi kuzingatiwa na klabu yoyote kwa sababu hawezi kuondoka.”
Romano aliongeza kuwa Osimhen ana furaha sana nchini Uturuki na klabu hiyo inajivunia kuwa na wachezaji wakubwa kama yeye, Rafael Leao, na Leroy Sane. Alieleza kuwa uvumi uliokuwa ukisambaa huenda ulitokana na mazungumzo kati ya Arsenal na Galatasaray kuhusu mshambuliaji Gabriel Martinelli, ambaye hata hivyo hakuwa tayari kwenda Uturuki.
Kwa hali hii, inaonekana Arsenal huenda ikabaki na kikosi ilichonacho kwa sasa ikiwa hawatafanikiwa kupata mbadala mwingine kabla ya muda wa usajili kumalizika.