Fabrizio Romano: Milango imefungwa, Tchouameni hataenda Manchester United
Milango imefungwa kwa Aurelien Tchouameni
Ndoto za Manchester United kumsajili kiungo mahiri wa Real Madrid, Aurelien Tchouameni, zimefika mwisho rasmi baada ya mtaalamu wa masuala ya usajili, Fabrizio Romano, kutoa tamko la mwisho kuhusu mustakabali wa mchezaji huyo.
Kwa muda mrefu, Manchester United imekuwa ikihusishwa kwa karibu na kiungo huyo wa kimataifa wa Ufaransa, ikimwona kama mbadala sahihi wa Casemiro na kiungo anayeweza kuimarisha kikosi cha kocha Michael Carrick. Hata hivyo, inaonekana juhudi hizo hazitazaa matunda msimu huu.
Mkataba mpya ndio mwisho wa tetesi
Akizungumza kupitia chaneli yake ya YouTube, Romano alisisitiza kuwa hakuna uwezekano wa Tchouameni kuondoka Santiago Bernabeu. Licha ya kuwepo kwa minong’ono ya hapa na pale, ukweli ni kwamba mchezaji huyo ameshakamilisha makubaliano ya kusalia klabuni hapo.
“United walikuwa wakimfikiria Tchouameni, lakini hilo lilikuwa kabla ya mkataba mpya. Walikuwa wakimwona kama chaguo lao la ndoto katikati ya uwanja. Ni mchezaji wa kiwango cha juu, mwenye uzoefu wa kimataifa na amezoea kucheza kwenye kiwango cha juu kabisa.”
Romano aliongeza kuwa dili hilo limekamilika na halina mjadala:
“Tchouameni amesaini mkataba mpya Real Madrid. Jambo hilo limekwisha kamilika. Makubaliano yameshafungwa. Atakuwa sehemu muhimu ya kikosi cha Jose Mourinho msimu ujao. Mchezaji ana imani kubwa na mradi wa klabu, hivyo Real Madrid na Tchouameni wataendelea kuwa pamoja.”
Hali ya mambo Old Trafford
Manchester United tayari imeshamaliza usajili wa viungo Andrey Santos na Youri Tielemans msimu huu. Pamoja na hayo, benchi la ufundi la ‘Mashetani Wekundu’ limekuwa likitafuta kiungo mwingine mmoja ili kuongeza nguvu katika kampeni yao ya kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya England na kufanya vizuri katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Ulaya.
Awali, kulikuwa na taarifa kutoka kwa wachambuzi mbalimbali kama Andy Mitten wakidokeza kuwa Real Madrid huenda ikalazimika kuuza mchezaji mkubwa ili kupata fedha za kufanya usajili wao, jambo ambalo lilitoa mwanya wa matumaini kwa United. Hata hivyo, kwa sasa, inaonekana suala hilo limezima rasmi.
Kwa sasa, mashabiki wa Manchester United watalazimika kuelekeza mawazo yao kwa malengo mengine ya usajili, kwani Tchouameni anasalia kuwa mali ya Real Madrid chini ya utawala wa Jose Mourinho.