FIFA yalaumiwa vikali kwa uamuzi wa kumruhusu Balogun kucheza Kombe la Dunia
Mgogoro wa Balogun watingisha Kombe la Dunia
Kombe la Dunia limeingia katika mtafaruku mkubwa baada ya FIFA kuchukua uamuzi wa kushangaza wa kusimamisha adhabu ya kadi nyekundu iliyokuwa ikimkabili mshambuliaji wa timu ya taifa ya Marekani, Folarin Balogun. Uamuzi huu umekuja kufuatia mazungumzo ya simu kati ya Rais wa Marekani, Donald Trump, na Rais wa FIFA, Gianni Infantino.
Balogun alikuwa amepewa kadi nyekundu katika mchezo dhidi ya Bosnia na Herzegovina baada ya kumchezea rafu mbaya mlinzi Tarik Muharemovic. Hata hivyo, badala ya kutumikia adhabu ya kawaida ya mchezo mmoja, FIFA imetangaza kusimamisha adhabu hiyo kwa kipindi cha mwaka mmoja wa majaribio, hatua inayomruhusu mchezaji huyo kuendelea na michuano hiyo.
UEFA watoa tamko zito
Umoja wa Mashirikisho ya Soka barani Ulaya (UEFA) haukufurahishwa na hatua hiyo ya FIFA, ukieleza bayana kuwa uamuzi huo unaharibu taswira ya ushindani na uadilifu wa mchezo. Katika taarifa yao, UEFA walisema:
“Tunaelezea kusikitishwa kwetu na uamuzi huu usio na kifani, usioeleweka na ambao hauna mashiko. Pale ambapo uhakika wa sheria hautolewi tena na walinzi wake, uadilifu wa mchezo unakuwa hatarini na kuaminika kwa michuano kunapungua.”
UEFA wameongeza kuwa kitendo hicho kinajenga utamaduni mbaya ambapo kila timu itataka haki sawa pindi matukio ya namna hiyo yanapojitokeza, jambo ambalo linaweza kuleta mkanganyiko mkubwa katika michuano hii.
Makocha na mashirikisho waonyesha tahadhari
Kocha wa England, Thomas Tuchel, ni miongoni mwa walioonyesha kushangazwa na mchakato huo. Akizungumza na waandishi wa habari, Tuchel alihoji misingi iliyotumika kubadili maamuzi hayo:
“Nani anafuta uamuzi huu na lini? Na kwa misingi ipi? Hii ni ya ajabu kwangu. Wapi mambo haya yanaanzia na wapi yanaishia?”
Kwa upande wake, Shirikisho la Soka la Ubelgiji (RBFA) limeelezea kushangazwa na uamuzi huo wa FIFA, likisisitiza kuwa hatua hiyo inapingana moja kwa moja na kanuni za michuano hiyo, huku wakisema wanaendelea kufuatilia suala hilo.
FIFA yafafanua msimamo wake
FIFA imejitetea kwa kurejea kifungu cha 27 cha Kanuni zake za Nidhamu, ikisema kuwa chombo chao cha kimahakama kina mamlaka ya kusimamisha utekelezaji wa adhabu kwa sehemu au kikamilifu. Kwa mujibu wa FIFA, Balogun yuko huru kucheza, lakini akifanya kosa lingine la namna hiyo ndani ya mwaka mmoja, adhabu yake ya awali itarudi na kuongezewa nyingine.
Rais Donald Trump kupitia mtandao wake wa Truth Social, alishukuru FIFA kwa kufanya “kitu sahihi” na kurekebisha kile alichokiita “dhuluma kubwa.” Wakati huo huo, kocha wa Marekani, Mauricio Pochettino, amekaribisha uamuzi huo akidai kuwa asilimia kubwa ya watu waliona adhabu hiyo ya kadi nyekundu ilikuwa isiyo ya haki.