Gabriel Martinelli kuhusishwa na uwezekano wa kuondoka Arsenal
Martinelli kutafuta changamoto mpya?
Winga wa Arsenal, Gabriel Martinelli, anadaiwa kuwa miongoni mwa wachezaji wanaotamani kuondoka kwenye klabu hiyo kabla ya dirisha la usajili kufungwa. Habari hizi zinakuja katika kipindi ambacho washika bunduki hao wa London wanajaribu kusuka upya kikosi chao baada ya kushinda taji la Ligi Kuu ya Uingereza msimu uliopita.
Kwa mujibu wa mchambuzi wa mambo ya kifedha katika soka, Stefan Borson, Martinelli ni mmoja wa wachezaji ambao wanaweza kuwa katika hatua inayofuata ya mauzo ya wachezaji ndani ya klabu hiyo. Hata hivyo, kizuizi kikubwa kinaonekana kuwa thamani ya mchezaji huyo, ambayo inatajwa kufikia paundi milioni 50.
“Kuna wachezaji ambao wataondoka. Kwa Arsenal, ni kama watu kama Gabriel Martinelli, ambao kimsingi wangependa kuondoka. Nadhani hiyo ndiyo hatua inayofuata ya usajili itakayotokea,” alisema Borson.
Ujio wa Vinicius Junior unaweza kuchochea mabadiliko
Tetesi za kuondoka kwa Martinelli zimepamba moto kufuatia kuripotiwa kwa jitihada za Arsenal kumleta staa wa Real Madrid, Vinicius Junior. Wachambuzi wengi wanaamini kuwa kama dili hilo litakamilika, nafasi ya Martinelli kikosini inaweza kuwa finyu, jambo linaloweza kumlazimisha kutafuta nafasi ya kucheza mara kwa mara klabu nyingine.
Bryan King, ambaye ni mchambuzi wa soka na aliyewahi kuwa skauti wa klabu kadhaa za Ligi Kuu ya Uingereza, anaamini kuwa ujio wa Vinicius Junior utaleta changamoto kubwa kwa Martinelli.
“Najiuliza Arsenal watafanya nini na Martinelli? Ni ngumu kwa sababu wana sifa zinazofanana uwanjani,” aliongeza King.
Je, Martinelli anataka kweli kuondoka?
Licha ya minong’ono hiyo ya soko la usajili, taarifa kutoka BBC Sport zinaeleza mtazamo tofauti. Inafahamika kuwa Martinelli, ambaye bado ana mkataba wa miaka miwili, ana furaha jijini London na hana haraka ya kuondoka klabuni hapo.
Inaelezwa kuwa Mbrazil huyo yuko tayari kusikiliza ofa tu ikiwa itakuwa ni fursa inayomfaa zaidi katika ukuaji wake wa soka, badala ya kulazimisha kuondoka bila mpango maalum. Kwa sasa, mashabiki wa Arsenal wanasubiri kuona hatua gani klabu yao itachukua, hususan katika eneo la ushambuliaji ambapo kocha Mikel Arteta anaonekana kutaka kuongeza nguvu zaidi kwa ajili ya msimu ujao.