Graeme Souness amvaa vibaya Declan Rice, adai kiungo huyo ana uwezo mdogo
Souness amtaja Rice kama mchezaji ‘mwenye mipaka’
Gwiji wa soka wa Liverpool, Graeme Souness, ametoa maoni mazito kuhusu kiwango cha kiungo wa Arsenal na England, Declan Rice, akimwelezea kama mchezaji ambaye uwezo wake umefika mwisho (limited) na hawezi kuongeza kiwango zaidi kwa sasa.
Kauli hii inakuja mara baada ya England kuondoshwa kwenye michuano ya Kombe la Dunia, ambapo Rice alionekana kushindwa kuiongoza vyema safu ya kiungo ya ‘The Three Lions’. Souness anaamini kuwa umri wa miaka 27 alionao Rice ndio ukomo wa uwezo wake wa soka.
Rice anapaswa kucheza kama beki?
Souness hakusita kuonyesha kutoridhishwa kwake na mtindo wa Rice wa kucheza mpira, akimlinganisha na nyota wa Manchester City, Rodri. Kwa mujibu wa Souness, Rice anatumia muda mwingi kukimbia na mpira au kupiga pasi za pembeni badala ya kutafuta njia za kuumiza wapinzani kwa pasi za hatari.
“Declan Rice kwangu mimi ana mipaka. Unawasikia watu wakisema yeye ni mchezaji wa kiwango cha dunia… mimi nadhani anaweza akawa beki wa kati,” alisema Souness kupitia mahojiano na Sports Uncensored.
Souness aliongeza kuwa licha ya Rice kuwa na nidhamu ya hali ya juu, kujituma, na nguvu za mwili, bado anashindwa kusoma mchezo haraka na kufanya maamuzi sahihi katikati ya uwanja. Alisisitiza kuwa kukimbia na mpira mara kwa mara kwa kiungo ni ishara kuwa mchezaji huyo haoni picha nzima ya mchezo kwa haraka.
John Terry amkingia kifua Rice
Kauli hiyo ya Souness haikupokelewa vyema na wote, huku gwiji wa Chelsea, John Terry, akijitokeza kumtetea Rice na kusisitiza kuwa yeye ni mchezaji wa kiwango cha dunia.
“Nipo upande wa Declan Rice, naamini ni mchezaji wa kiwango cha dunia. Jukumu lake katika kikosi cha England siyo kukimbia mbele au kupiga pasi za kufungua ngome ya wapinzani, Declan ni kama Rodri, anazuia kila kitu kinachokuja mbele yake,” alijibu Terry.
Hata hivyo, Souness alisisitiza msimamo wake, akidai kuwa Rice na wachezaji wengine wa aina yake ni ‘steady Eddie’—wachezaji wanaocheza kwa wastani na wasio na uwezo wa kubadilisha matokeo ya mchezo kwa ubunifu (midfield maestros).
Rice, ambaye alikuwa nguzo muhimu katika safari ya Arsenal kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza msimu uliopita, alikumbwa na changamoto za majeraha na maradhi wakati wa michuano ya Kombe la Dunia, jambo ambalo lilimuathiri sana katika mechi za hatua za mtoano.