Guglielmo Vicario afunguka sababu za kuondoka Tottenham
Shukrani kwa De Zerbi
Kipa wa zamani wa Tottenham, Guglielmo Vicario, ameweka wazi hisia zake kufuatia kuondoka kwake klabuni hapo msimu huu wa joto. Kipa huyo raia wa Italia, ambaye kwa sasa anacheza kwa mkopo huko Juventus, amemshukuru kocha wake wa zamani, Roberto De Zerbi, kwa kuridhia ombi lake la kutaka kuondoka.
Vicario alionyesha heshima kubwa kwa De Zerbi kwa jinsi alivyoshughulikia mchakato wake wa kuondoka, akimsifu kocha huyo kuwa ni mtu wa maneno yake na mwenye msimamo thabiti.
“Uhusiano wetu ulikuwa mzuri tangu siku ya kwanza. Nilimshukuru binafsi siku nilipokamilisha usajili wangu na Juventus. Kwangu yeye alikuwa mtu wa kweli, mwazi na zaidi ya yote, mtu wa maneno yake. Alinipa fursa ya kupiga hatua niliyokuwa nimeipanga, aliniunga mkono na nitabaki kuwa mwenye shukrani kwake daima,” alisema Vicario katika mahojiano na Sky Sports Italia.
Changamoto za ndani Tottenham
Katika ufafanuzi wake, Vicario hakusita kugusia mazingira ya ndani ya klabu hiyo ambayo yalimfanya aone ni wakati sahihi wa kutafuta changamoto mpya. Licha ya kutotaka kuweka wazi kila undani, alidokeza kuwa mambo mengi hayakuwa yanaenda sawa ndani ya kikosi hicho.
“Kuna mambo kadhaa (dynamics) ambayo hayakuwa yameoana au kwenda sawa, na nadhani si busara kuyaweka hadharani kwa sasa,” aliongeza kipa huyo.
Maisha mapya Juventus
Baada ya kupata wakati mgumu mwishoni mwa msimu uliopita chini ya De Zerbi, ambapo alikosa nafasi ya kucheza katika michezo saba ya mwisho, Vicario anaonekana kurejesha furaha yake nchini Italia. Kwa sasa, Juventus wana chaguo la kumsajili kipa huyo jumla kwa ada ya pauni milioni 8.5.
Kuanzia kwake Juventus kumekuwa na matunda, ambapo amecheza michezo mitatu na kufanikiwa kutokuruhusu bao (clean sheet) katika michezo yake miwili ya kwanza dhidi ya Frosinone na Parma.
Kwa upande wa Tottenham, nafasi yake imechukuliwa na Antonin Kinsky ambaye amekuwa chaguo la kwanza katika michezo yote minne ya klabu hiyo msimu huu, huku Martin Dubravka akisajiliwa kama kipa mbadala.