Erling Haaland anza kuhusishwa na mpango wa kutua Barcelona
Haaland na mipango ya baadaye
Taarifa mpya kutoka nchini Hispania zimeibua mjadala mzito kuhusu mustakabali wa mshambuliaji matata wa Manchester City, Erling Haaland. Inaripotiwa kuwa kambi ya nyota huyo wa Norway imeshaanza mawasiliano na uongozi wa Barcelona kuhusu uwezekano wa kujiunga na klabu hiyo ya Catalan hapo baadaye.
Ripoti hizi zinakuja wakati ambapo Manchester City inakabiliwa na kipindi kigumu nje ya uwanja, kufuatia tuhuma za kukiuka kanuni za matumizi ya fedha (FFP) kati ya mwaka 2009 na 2018. Ingawa klabu hiyo imepanga kukata rufaa dhidi ya maamuzi hayo, hali ya kutokuwa na uhakika imewafanya wachezaji wengi kuanza kufikiria hatima zao.
Mawasiliano na uongozi wa Barca
Mwandishi wa habari kutoka Hispania, Juan Jesus, amedai kuwa timu ya usimamizi wa Haaland imemjulisha rais wa Barcelona, Joan Laporta, kuhusu gharama zinazohitajika ili kufanikisha dili hilo, ikiwemo ada ya uhamisho na mahitaji ya mshahara.
“Ninaweza kuthibitisha hili kwenu: kwa mara ya kwanza, watu wa karibu na Erling Haaland wamepiga hatua mbele kuhusiana na nia ya Barcelona. Timu ya mchezaji huyu imeiambia bodi ya Blaugrana kuhusu ada ya uhamisho inayokadiriwa na mahitaji ya mshahara kwa ajili ya dili la baadaye,” alieleza mwandishi huyo kupitia mtandao wa X.
Mkakati wa muda mrefu
Ingawa taarifa hizi zinaweza kuzua taharuki, mwandishi huyo alisisitiza kuwa Haaland bado ana furaha Manchester City na ana mkataba wa muda mrefu. Hata hivyo, hatua hiyo inaonekana kama maandalizi ya mpango wa muda mrefu. Inatajwa kuwa ikiwa Haaland ataamua kutafuta changamoto mpya, Barcelona ndiyo chaguo lake la kwanza kwa sababu ya mvuto wa ligi ya LaLiga na nafasi ya kuwa kiongozi wa mradi mpya wa klabu hiyo akicheza sambamba na Lamine Yamal.
Inafahamika kuwa Joan Laporta ana ndoto ya kufanya usajili mkubwa wa ‘Galactico’ wakati uwanja wa Spotify Camp Nou utakapokamilika kikamilifu kuelekea mwaka 2027 au 2028. Mbinu hii inafanana na ile iliyotumika kumpata Rodri, ambaye aliunganishwa na Barcelona miaka miwili kabla ya kutua klabuni hapo mwaka 2026.
Mtazamo wa Laporta
Laporta amekuwa akimfuatilia Haaland tangu alipokuwa Borussia Dortmund mwaka 2021. Kwa sasa, taarifa hizi hazimaanishi kuwa mchezaji huyo anaondoka Etihad katika dirisha lijalo, bali ni mchakato wa kawaida wa soka ambapo kambi ya mchezaji hufanya mawasiliano ya awali na klabu zinazovutiwa naye ili kuweka ramani ya baadaye wazi.