Skip to content

Hansi Flick afunguka kuondoka kwa Ronald Araujo kuelekea Liverpool

SokaNews
Updated: Published: Jumapili, 9 Agosti 2026 · 2 min read
barcelona liverpool ronaldaraujo hansiflick usajili laliga
Hansi Flick afunguka kuondoka kwa Ronald Araujo kuelekea Liverpool

Mabadiliko ya upepo ndani ya Barcelona

Kocha wa Barcelona, Hansi Flick, amethibitisha kuwa beki wake Ronald Araujo yupo hatua za mwisho kukamilisha uhamisho wake wa kwenda Liverpool kwa mkopo. Uamuzi huu unakuja huku klabu hizo zikikubaliana kuwa beki huyo mwenye umri wa miaka 27 anaweza kuwa na changamoto mpya kule Anfield.

Liverpool imelazimika sokoni kutafuta mbadala kutokana na majeraha yanayowakabili wachezaji wao wa safu ya ulinzi, wakiwemo Conor Bradley, Giovanni Leoni, na Joe Gomez. Inaripotiwa kuwa Liverpool ina chaguo la kumnunua jumla beki huyo wa Uruguay msimu ujao kwa ada ya pauni milioni 47.

Kwa nini Flick amemruhusu kuondoka?

Licha ya Araujo kuwa nahodha wa Barcelona msimu uliopita, mchango wake ulikuwa mdogo uwanjani kutokana na changamoto mbalimbali, ikiwemo afya ya akili iliyomfanya kukaa nje ya dimba kwa mwezi mmoja katikati ya msimu. Flick anakiri kuwa mchezaji huyo ana uwezo mkubwa lakini mfumo wake wa soka haumfiti vyema beki huyo.

“Nadhani Ronald ni mtu mzuri sana na mchezaji mahiri. Nadhani mtindo wetu wa soka ambao tunataka kuucheza ni tofauti kidogo. Ni mchezaji mwenye kasi, ana nguvu, na ni hodari sana kimwili na hata akiwa na mpira ana uwezo mzuri,” alisema Flick.

Kocha huyo Mjerumani aliongeza kuwa, “Hatukuweza kumjumuisha katika mipango yangu kama nilivyotaka, na nadhani anahitaji kuanza kitu kipya. Kile kilichotokea huko nyuma kiliathiri sana hali yake. Nilimuona asubuhi hii na kumuaga, naona alikuwa na furaha sana, na Liverpool ni klabu nzuri. Namtakia kila la heri kwa sababu anastahili. Ni mtu na mchezaji bora aliyekuwa nahodha mzuri.”

Changamoto ya Araujo kabla ya kuondoka

Safari ya Araujo kuelekea Liverpool inakuja baada ya kipindi kigumu alichokipitia Barcelona. Msimu uliopita alicheza mechi 11 pekee za La Liga. Hapo awali, beki huyo aliwahi kuweka wazi mapambano yake dhidi ya msongo wa mawazo na unyogovu (depression) baada ya kupewa kadi nyekundu kwenye mchezo wa Ligi ya Mabingwa dhidi ya Chelsea mwezi Novemba.

Alipozungumzia hali hiyo mwezi Februari, Araujo alikiri: “Nilikuwa nikipambana na wasiwasi (anxiety) kwa mwaka mmoja na nusu ambao uligeuka kuwa unyogovu, na nilikuwa nikicheza katika hali hiyo. Hilo halisaidii, kwa sababu uwanjani hujihisi kama wewe mwenyewe.”

Sasa, Liverpool wanatarajia kumtumia beki huyo mahiri katika nafasi ya ulinzi wa kati na hata kama beki wa kulia, huku mashabiki wakisubiri kuona kama atafanikiwa kurudisha kiwango chake cha juu katika ligi ya England.