Skip to content

Harry Kane avunja ukimya baada ya England kutolewa Kombe la Dunia

SokaNews
Updated: Published: Jumatano, 15 Julai 2026 · 2 min read
england harrykane argentina thomastuchel kombeladunia
Harry Kane avunja ukimya baada ya England kutolewa Kombe la Dunia

Ndoto ya England kuyeyuka nusu fainali

Nahodha wa timu ya taifa ya England, Harry Kane, amesema wamejawa na huzuni kubwa baada ya timu hiyo kupoteza mchezo wa nusu fainali ya Kombe la Dunia dhidi ya Argentina, licha ya kutangulia kufunga bao katika mchezo huo uliofanyika Jumatano.

England ilionekana kuwa na matumaini makubwa baada ya Anthony Gordon kuwapa bao la kuongoza katika dakika ya 55. Hata hivyo, shinikizo kubwa kutoka kwa Argentina lilizaa matunda, Enzo Fernandez akisawazisha kabla ya Lautaro Martinez kupiga bao la ushindi katika dakika za nyongeza.

Ujumbe wa Thomas Tuchel ulikuwa nini?

Kumekuwa na mjadala mkubwa kuhusu mbinu zilizotumiwa na kocha Thomas Tuchel baada ya England kufunga bao. Mashabiki wengi wamemnyooshea kidole kocha huyo kwa kudai kuwa kikosi kilijilinda kupita kiasi badala ya kusaka bao la pili.

Akijibu tuhuma hizo, Kane alisisitiza kuwa maelekezo yaliyotolewa na benchi la ufundi yalikuwa wazi:

“Wakati tunapata bao la kuongoza, ujumbe ulikuwa ni tuendelee kushambulia na kusaka bao lingine. Lakini baada ya wao kusawazisha na kuongeza la pili, ilikuwa vigumu kurudisha hali ya mchezo kwetu,” alisema Kane.

Tuchel atetea maamuzi yake

Kocha Thomas Tuchel amekubali kubebe jukumu la matokeo hayo, lakini amesisitiza kuwa hana majuto kwa maamuzi aliyoyafanya uwanjani. Alieleza kuwa tatizo halikuwa la kimfumo, bali timu ilijikuta ikicheza kwa tahadhari (passive) kadiri muda ulivyozidi kuyoyoma.

“Tulitaka bao la pili, lakini sikuona kama kufanya mabadiliko ya washambuliaji yangeleta msaada. Tulibaki kwenye mfumo wetu wa 4-4-2, lakini tukaanza kucheza kwa tahadhari na kushindwa kumiliki mpira. Sio tatizo la kimfumo, lakini nakubali kuwajibika kama kocha,” alisema Tuchel.

Safari inaishia hapa

England imekuwa ikisaka taji la Kombe la Dunia tangu waliposhinda mwaka 1966, lakini safari hii wameishia nusu fainali. Kane aliongeza kuwa licha ya maumivu ya kufungwa, anajivunia jitihada za wachezaji wenzake.

“Tumefanya kazi kubwa na tumecheza kwa jasho na damu. Tuna vipindi vizuri katika mashindano haya, lakini bado tunahitaji kutafuta kile kitu kinachokosekana ili kufika hatua ya mwisho,” alihitimisha nahodha huyo.