Hatima ya Sheikh Mansour ndani ya Man City baada ya tuhuma za FFP
Mgogoro wa FFP na hatima ya uongozi wa Manchester City
Wakati klabu ya Manchester City ikikabiliwa na kipindi kigumu baada ya kukutwa na hatia ya kukiuka kanuni za matumizi ya fedha (FFP) kwa kipindi cha kuanzia mwaka 2009 hadi 2018, mjadala mkubwa umeibuka kuhusu hatima ya mmiliki wa klabu hiyo, Sheikh Mansour.
Katika kipindi cha The Overlap, mwandishi wa habari za michezo kutoka The Athletic, David Ornstein, alijibu maswali mazito yaliyoibuliwa na mchambuzi Jamie Carragher kuhusu kama kuna uwezekano wa wamiliki wa sasa wa klabu hiyo kuondolewa madarakani kufuatia sakata hilo linaloendelea kuitikisa Premier League.
Je, Sheikh Mansour anaweza kuondolewa?
Carragher alitoa maoni kuwa kutokana na ukubwa wa tuhuma hizo, uongozi wa sasa wa Manchester City unapaswa kuondoka ili klabu ianze upya. Hata hivyo, Ornstein alisisitiza kuwa mambo hayafanyi kazi kwa namna ya matamanio ya nje, bali yanafuata taratibu za kisheria.
Ornstein alieleza kuwa kuondolewa kwa mmiliki ni jambo ambalo lingehitaji uamuzi kutoka kwa mdhibiti huru (independent regulator). Alisema:
“Ili jambo hilo lifanikiwe, ni lazima mdhibiti huru athibitishe kuwa wamiliki hao hawana sifa za kuendelea kuongoza klabu (fit and proper owners and directors).”
Ufafanuzi kuhusu ripoti ya kamati huru
Jambo moja lililozua mjadala ni sehemu ya ripoti iliyofichwa (redacted) ambayo inamtaja mtu ambaye hakufahamu kuhusu ufadhili wa mikataba ya klabu hiyo. Kumeibuka dhana kuwa mtu huyo huenda ni Sheikh Mansour mwenyewe.
Ornstein aliongeza kuwa kama ikithibitika kuwa Sheikh Mansour hakuhusika moja kwa moja na uvunjifu huo wa sheria, basi hatua za kinidhamu huenda zikaelekezwa kwa watendaji wakuu wa klabu waliokuwa wakisimamia shughuli hizo wakati makosa hayo yakitokea.
Mustakabali wa adhabu kwa City
Wakati klabu hiyo ikipanga kukata rufaa dhidi ya uamuzi wa kamati huru, Ornstein alikiri kuwa ni vigumu kutabiri adhabu hasa ambayo Manchester City itapewa, kwani jambo hili halijawahi kutokea kwa ukubwa huu.
“Upeo mzima wa adhabu upo wazi kwa kamati huru; inaweza kuwa adhabu ndogo au madhara makubwa sana kwa Manchester City. Kwa kuzingatia kuwa wamepatikana na hatia ya mashtaka yote ya kifedha, ungetarajia adhabu itakuwa nzito sana,” alisema Ornstein.
Kwa sasa, ulimwengu wa soka unasubiri kuona hatua zitakazofuata huku klabu hiyo ikiendelea kupambana kisheria kulinda heshima yake.