Ismaila Sarr ataka kuondoka Crystal Palace, Liverpool yashinikiza kumsajili
Mvutano wa usajili Anfield na Selhurst Park
Staa wa Senegal na klabu ya Crystal Palace, Ismaila Sarr, ameripotiwa kuwa kwenye wakati mgumu wa kisaikolojia baada ya ofa ya pili ya Liverpool kwa ajili ya huduma yake kukataliwa na klabu hiyo ya London.
Liverpool wamekuwa wakimnyatia winga huyo kwa muda sasa, wakitaka kuziba nafasi iliyoachwa wazi na Cody Gakpo anayehusishwa na kutaka kujiunga na Manchester City. Hata hivyo, Crystal Palace wameonekana kuwa wagumu kuachia nyota huyo, wakitaka kiasi cha pauni milioni 75 ili kumruhusu kuondoka.
Sarr agoma kufanya mazoezi
Hali imekuwa mbaya kuelekea kufungwa kwa dirisha la usajili, huku taarifa kutoka kwa waandishi mbalimbali barani Ulaya zikithibitisha kuwa Sarr amechukua uamuzi mzito wa kugoma kufanya mazoezi na wenzake.
Mwandishi wa habari za michezo, Santi Aouna, ameeleza kuwa mchezaji huyo amefikia hatua hiyo ili kuishinikiza klabu yake imruhusu kutimkia Anfield. Aouna aliandika kwenye mtandao wake:
“Crystal Palace wanadai pauni milioni 75 kutoka kwa Liverpool kwa ajili ya Ismaila Sarr. Klabu hiyo ya London haifurahishwi na ulazima wa kumuuza mchezaji wake katika siku za mwisho za dirisha la usajili, hivyo wanachelewesha mazungumzo ili kupandisha bei.”
Msimamo wa Liverpool na Sarr
Kwa upande wake, mwandishi wa RMC Sport, Fabrice Hawkins, amethibitisha kuwa Sarr amedhamiria kujiunga na Liverpool kwa gharama yoyote. Hawkins alibainisha kuwa winga huyo hataki tena kuvaa jezi ya Crystal Palace.
“Crystal Palace wamekataa ofa ya pili kutoka Liverpool kwa ajili ya Ismaïla Sarr. Mchezaji huyo anataka kuondoka na kujiunga na Liverpool kwa gharama yoyote. Sarr hatashiriki mazoezi leo wakati akishinikiza uhamisho huo na hataki tena kuvaa jezi ya Crystal Palace.”
Sarr, ambaye amekuwa na mafanikio makubwa tangu ajiunge na Palace mwaka 2024, ikiwemo kushinda kombe la FA, Community Shield, na Conference League, anaamini kuwa muda wake wa kutafuta changamoto mpya umefika.
Wakati Liverpool wakijaribu kila mbinu kukamilisha dili hili kabla ya dirisha kufungwa siku ya Jumanne, bado kuna sintofahamu kuhusu hatima ya Cody Gakpo, ambaye anatarajiwa kubaki klabuni hapo iwapo mpango wa kumnunua Sarr utashindikana.